Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi maadhimisho siku ya vijana duniani kitaifa mkoani Shinyanga Emmanuel Ntobi akizungumza na waandishi wa habari, (kushoto) Mwenyekiti wa BAVICHA Kata ya Ngokolo Stephano Wilibert, (kulia) ni Mwenyekiti wa Chadema Kata ya Ngokolo Yohana Munisa.
Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi maadhimisho siku ya vijana duniani kitaifa mkoani Shinyanga Emmanuel Ntobi akizungumza na waandishi wa habari huku akiwa ameshika Sera ya Vijana ya Chadema (kushoto) Mwenyekiti wa BAVICHA Kata ya Ngokolo Stephano Wilibert, (kulia) ni Mwenyekiti wa Chadema Kata ya Ngokolo Yohana Munisa.
Na Marco Maduhu, SHINYANGA
CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kinatarajia kufanya maadhimisho ya siku ya vijana duniani ambayo kitaifa yatafanyika mkoani Shinyanga.
Maadhimisho hayo yatafanyika Agost 12 mwaka huu, ambayo yameandaliwa na Baraza la vijana wa Chadema (BAVICHA), huku Mgeni Rasmi akitarajiwa kuwa ni Mwenyekiti wa Chadema Taifa Freman Mbowe.
Mwenyekiti wa Kamati wa maandalizi maadhimisho ya siku ya vijana duniani mkoani Shinyanga Emmanuel Ntobi, amebainisha hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye Ofisi za Chadema Kanda ya Serengeti mkoani humo.
Amesema Chadema ni chama ambacho kina heshimu na kufuata misingi ya kidemokrasia pamoja na uhuru wa makundi mbalimbali ya kijamii yakiwamo ya vijana, ndiyo maana wameamua kuadhimisha siku hiyo ya vijana duniani na haijawahi kutokea hapa nchini.
“Siku ya vijana Duniani ilianzishwa na Umoja wa Mataifa Agost 2020, na kupata azimio namba 54, kuwa kutakuwa na siku ya vijana duniani na itaadhimishiwa kila mwaka Agost 12, na kutoa fursa kwa Serikali na Taasisi nyingine na kuweka muangalizo wa masuala ya vijana ulimwenguni,”amesema Ntobi
“Maadhimisho hayo huambatana na Matamasha, Warsha, hafla za kitamaduni, mikutano inayohusisha vyama vya siasa, maafisa wa Serikali na Mashirika ya vijana, na kutakuwa na kujadili mambo mbalimbali kwa ajili ya mustakabali wa maisha ya vijana,”ameongeza.
Ntobi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Shinyanga, amesema katika siku hiyo ya maadhimisho ya vijana kitaifa mkoani humo, wanatarajia kuwa na wageni vijana zaidi ya 4,000, na kutoa wito kwa wafanyabiashara mkoani humo kuchangamkia fursa hiyo kujikwamua kiuchumi.