Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Tarehe 23 mwezi Agosti mwaka huu Watanzaia nchi nzima wanatarajia kushiriki katika zoezi la sensa ya watu. Kufanikiwa kwa zoezi hili kunategemea sana ushiriki wa waandishi na vyombo vya habari kuelimisha na kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kuhesabiwa.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele kuhimiza uhamasishaji na uelimishaji wananchi kuhusu umuhimu wa sensa kwa maendeleo ya taifa.
“Uelimishaji na uhamasishaji ni masuala yanayotakiwa kupewa kipaumbele ili kuwasaidia wananchi kutoa taarifa kwa ajili ya kuiwezesha serikali kupata takwimu sahihi zitakazoiwezesha kupanga mipango ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii” alisisitiza Mhe. Rais Samia wakati akizindua Nembo na tarehe ya sensa jijini Dar es Salaam.
Ingawa kumekuwepo na jitihada za uhamasishaji na uelimishaji wananchi kuhusu zoezi hilo kupitia maudhui ya vyombo vya habari na jumbe zinazosambazwa kwa njia ya simu, bado vyombo vya habari havijaweka msisitizo wa kutosha katika zoezi hili muhimu.
Hii imejidhihirisha katika uhaba wa maudhui yanayoelimisha na kuhamasisha wananchi masuala ya sensa yanayozalishwa na vyombo vya habari vyenyewe. Hali hii inanyima wananchi haki ya kupata taarifa zitakazowawezesha kufanya maamuzi sahihi ya kushiriki na kutoa taarifa zao wakati wa utekelezaji wa zoezi la sensa mwezi ujao.
Vyombo vya habari vina wajibu wa kushirikiana na Serikali katika kuwaongezea uelewa wananchi kuhusu umuhimu wa sensa kwa maendeleo.
Ni muhimu, angalau kwa kipindi kilichosalia zoezi la sensa liwe agenda kuu inayotawala maudhui ya vyombo vyote vya habari nchini.
Kuibeba agenda hii kutatoa fursa kwa wananchi wengi sio tu kupata taarifa bali pia kuwawezesha kutoa maoni, kuuliza maswali na kutaka ufafanuzi wa masuala mbalimbali kuhusu sensa kupitia vyombo na majukwaa ya kihabari.
Kwa kufanya hivi kutapanua wigo wa upatikanaji wa taarifa mbalimbali za sensa.
Ikumbukwe kwamba zoezi la sensa ya watu na makazi nchini Tanzania lilianza kutekelezwa kwa mara ya kwanza mwaka 1967 na kuendelea mwaka 1978, 1988, 2002, 2012 na hili linalotarajiwa kufanyika Agosti 23 mwaka huu 2022.
Sensa inalenga kujua idadi ya watu kwa kuzingatia vigezo kadha wa kadha ikiwemo umri, jinsia, mahali walipo, kiwango cha elimu, ajira na makazi.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464