LIGI KUU YA NETIBOLI KUUNGURUMA KUANZIA KESHO

Mwenyekiti wa CHANETA, Dkt. Devotha Marwa, akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam katika Hoteli ya Serena, ambapo ametangaza kuanza kwa Ligi Kuu ya mchezo wa pete nchini.

**************************
-CHANETA yaweka historia kwa ushiriki wa timu 29 kwenye ligi
-Yatambulisha wadhamini na kutoa wito kwa taasisi binafsi na za umma kujitokeza

Dar es Salaam, Julai 8, 2022

CHAMA Cha Netiboli Tanzania (CHANETA) kimetangaza kuwa Ligi Daraja la Kwanza la Klabu Bingwa ya Netiboli nchini itaanza tarehe 9 Julai hadi tarehe 19 Julai mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Ligi hiyo kwa mara ya kwanza katika historia ya mchezo wa pete nchini itashirikisha jumla ya timu 29, amacho ni kiwango kikubwa cha ushiriki wa timu kuwahi kutokea.

Kamati ya Utendaji ya CHANETA ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Dk Devotha Marwa, imetangaza kuwa mashindano hayo yatafanyika kwenye Uwanja wa Ndani (Indoor Stadium) Jijini Dar es Salaam.

"Ligi Kuu ya Netiboli ina malengo makuu matatu. Lengo la kwanza ni kutoa wachezaji wanaoenda kuunda Timu ya Taifa ya Netiboli, maarufu kama Taifa Queens, inayotuwakilisha kwenye mashindano ya netiboli yanayofanyika sehemu mbalimbali, ikiwemo kufuzu kwenye mashindano ya Kombe la Dunia yatakayofanyika Afrika ya Kusini," Marwa amesema kwenye mkutano wa waandishi wa habari katika hoteli ya Serena, Dar es Salaam.

"Lengo la pili ni kupata washindi watatu wa kwanza ambao wataliwakilisha taifa kwenye Mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati na lengo la tatu likiwa kupata Timu Bora 6 ambazo zitashiriki kwenye Mashindano ya Kombe la Muungano," amesema.

Naye Katibu Mkuu wa CHANETA, Rose Mkissi, alitoa wito kwa taasisi za umma na binafsi kujitokeza kudhamini mashindano hayo ya Ligi Kuu ya Netiboli nchini ambayo yanafanyika Dar es Salaam.

Dkt. Marwa pamoja na uongozi mpya wa CHANETA, chini ya Makamu Mwenyekiti Shy-Rose Bhanji na Katibu Mkuu Rose Mkisi wameleta muamko mpya wa mchezo wa pete nchini.

Kauli mpya ya CHANETA, "Netiboli Mwanzo Mpya," inalenga kufufua mchezo huo ambao umekuwepo nchini tangu miaka ya 1960.

Timu zitazoshiriki mashindano ya Ligi Kuu Daraja la Kwanza la Netiboli zinatoka mikoa mbalimbali nchini, ikiwemo Dar es Salaam, Dodoma, Kigoma na kona nyingine za nchi.

Wakati huo huo, CHANETA imetangaza baadhi ya wadhamini wake kwenye Ligi Kuu ya Netiboli ya mwaka huu.

Wadhamini hao ni Benki ya NMB na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Hoteli ya Serena, Chama Cha Msalaba Mwekundu Tanzania na Kampuni ya Maji ya Hill Water.

Wadhamini wengine wanatarajiwa kutangazwa rasmi na CHANETA baada ya kuthibitisha udhamini wao wa mashindano hayo.

Mkutano huo wa waandishi wa habari umehudhuriwa na wajumbe kadhaa wa Kamati Tendaji ya CHANETA na mshauri wa chama hicho, Betty Mkwasa.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464