MADHARA KUOGESHA DAWA MVUTO WA MAPENZI ‘SAMBA­’ MWANAFUNZI ADAIWA KUAMBUKIZWA VIRUSI VYA UKIMWI SHINYANGA



Na Marco Maduhu, SHINYANGA

MWANAFUNZI ambaye jina lake limehifadhiwa Mkazi wa Kata ya Ilola wilayani Shinyanga, amedaiwa kuambukizwa virusi vya ukimwi baada ya kuozeshwa ndoa ya utotoni.


Mwanafunzi huyo imeelezwa aliogeshwa dawa ya mvuto wa mapenzi maarufu Samba na wazazi wake ili apate mume wa kumuoa kwa lengo la wao kupata mifugo.

Mratibu wa Miradi kutoka Shirika la Rafiki-SDO mkoani Shinyanga Mariamu Maduhu, amebainisha hayo jana wakati akiwasilisha taarifa ya tathimini ya ufungaji wa mradi wa kupinga matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto wilayani Shinyanga.

Amesema wakati wa utekelezaji wa mradi huo, wamekumbana na Changamoto ya baadhi ya wazazi kwenye Kata hiyo ya Ilola, kuwaogesha watoto wao wa kike dawa ya mvuto wa mapenzi maarufu Samba ili wapate wanaume wa kuwaoa na kupata utajiri wa mifugo.

"Wakati wa utekelezaji wa mradi tumekumbana na Mwanafunzi ambaye aliogeshwa dawa ya mvuto wa mapenzi na wazazi wake 'Samba' akaolewa na kuacha masomo, lakini hakudumu kwenye ndoa yake akaachika huku tayari akiwa amesha ambukizwa Virusi vya Ukimwi," amesema Maduhu

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wilayani Shinyanga Deus Mhoja, amesema jamii bado inapaswa kuendelea kupewa elimu juu ya masuala ya kupinga ukatili hasa kwa watoto, ambao ndiyo waathirika wakubwa na hata kuzima ndoto zao.

Alisema matukio ya ukatili dhidi ya watoto na wanawake wilayani humo bado yapo, lakini yamepungua kwa kiasi kikubwa kutokana wadau mbalimbali kuendelea kutoa elimu, pamoja na wahusika kuchukuliwa hatua wakiwamo wazazi na watia mimba.

Aidha, amesema Serikali katika mwaka wa fedha (2022-2023) Idara yao ya Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri hiyo imetengewa kiasi cha fedha Sh.milioni 20, kwa ajili ya mapambano ya kupinga ukatili kwa watoto na wanawake .

Naye Mratibu wa Mfuko wa Ruzuku wa wanawake Tanzania (WFT-Trust) mkoani Shinyanga Glory Mbia, ambao wametoa ufadhili wa fedha kwa wadau kutekeleza mradi wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto wilayani Shinyanga, amesema licha ya mradi huo kuisha Serikali inapaswa kuendeleza mapambano hayo na kumaliza kabisa ukatili ndani ya Jamii.


Mratibu wa Miradi kutoka Shirika la Rafiki- SDO Mariamu Maduhu akiwasilisha taarifa ya mradi wa kupinga ukatili wa kijinsia Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wakati wa kufunga mradi huo.

Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Halmsahuri ya wilaya ya Shinyanga Deus Mhoja akizungumza kwenye kikao hicho.

Mratibu wa mfuko wa Ruzuku wa wanawake Tanzania (WFT-Trust) mkoani Shinyanga Glory Mbia akizungumza kwenye kikao hicho.

Waandishi wa habari kutoka mkoani Shinyanga ambao nao walikuwa wanufaika wa mradi huo wakiwa kwenye kikao hicho cha kufunga mradi.

kikao cha kufunga mradi kikiendelea.

kikao cha kufunga mradi kikiendelea.
Picha ya pamoja ikipigwa mara baada ya kumalizika kwa kikao cha kufunga mradi.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464