MAKATIBU WAKUU WATEMBELEA UJENZI KIWANDA BOMBA LA MAFUTA, WAHIMIZA WATANZANIA KUCHANGAMKIA FURSA KUJIKWAMUA KIUCHUMI

Makatibu Wakuu kutoka Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Wizara ya Nishati, wakiwa na viongozi mbalimbali kwenye kiwanda cha bomba la mafuta, cha mfumo wa kupasha Joto Mafuta katika kijiji cha Sojo Kata ya Igusule wilayani Nzega.

Na Marco Maduhu. NZEGA

Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Fedha na Mipango Emmanuel Tutuba, na Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Nishati Mhandisi Felchesmi Mramba, wametembelea ujenzi wa kiwanda cha Bomba la Mafuta kilichopo kijiji cha Sojo Kata ya Igusule wilayani Nzega, ambacho kitatumika kupasha mafuta Joto.

Makatibu hao wamefanya ziara hiyo leo Julai 7, 2022 wakiwa wameambatana na wataalum kutoka Wizara ya Nishati, pamoja na viongozi kutoka wilaya ya Nzega akiwamo Mkuu wa wilaya hiyo (ACP) Advera Bulimba.

Akizungumza kwenye ziara hiyo Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Fedha na Mipango Emmanuel Tutuba, amesema Serikali ya Tanzania imewekeza Hisa asilimia 15 kwenye mradi huo wa Bomba la Mafuta, ambalo linatoka Nchini Uganda hadi Tanga na mradi huo una gharama ya Sh. Trilioni 11.8.

Anasema tayari Serikali ya Tanzania imeshatoa fedha Taslimu kwenye mradi huo asilimia 40, na ndiyo maana wameamua kufanya ziara ili kuona utekelezaji na maendeleo ya ujenzi wa mradi wa bomba hilo la mafuta.

“Kwenye mradi huu wa bomba la mafuta Serikali ya Tanzania tuna Hisa asilimia 15 na tayari tumeshatoa kiasi cha fedha, na ndiyo maana tunafuatilia ili kuona maendeleo ya ujenzi wa mradi huu, ambao unafaida kubwa kwa Watanzania kiuchumi,” amesema Tutuba

“Natoa wito kwa Watanzania wajitokeze kwa wingi kuchangamkia fursa za ajira kwenye mradi huu wa bomba la mafuta, kuuza vyakula, na kupata zabuni ya kusambaza vifaa vya ujenzi sababu kazi hiyo inafanywa na Watanzania,”ameongeza.

Naye Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Nishati Mhandisi Felchesmi Mramba, amesema ujenzi wa mradi huo wa bomba la mafuta ni wa miaka mitatu, na ulianza Rasmi Februari mwaka huu mara baada ya kumaliza kusainiwa nchini Uganda na utatoa ajira nyingi kwa vijana.

Amesema katika ujenzi wa mradi huo, maeneo yote ambayo wananchi wamepitiwa na bomba hilo la mafuta tayari wameshalipwa fidia pamoja na wengine kujengewa nyumba sehemu zingine.

Katika hatua nyingine amewatoa wasiwasi Watanzania, kuwa kwenye mradi huo wa bomba la mafuta hakutakuwa na uharibifu wowote wa Mazingira, bali wamejipanga vyema kuhakikisha mazingira yanabaki kuwa salama.

Aidha, Kaimu Meneja wa kiwanda hicho cha Mfumo wa kupasha Mafuta Joto Wiliam Kajagi, amesema kwa sasa ujenzi huo upo katika hatua za awali na unaendelea vizuri.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Nzega (ACP) Advera Bulimba, amesema ujenzi wa kiwanda hicho upo salama, na hakuna malalamiko yoyote kutoka kwa wananchi, huku akimpongeza Rais Samia Suluhu Hassani kwa kupeleka ujenzi wa kiwanda hicho wilayani humo ambapo wananchi wake wananufaika nao kiuchumi.

Nao baadhi ya wananchi wa eneo hilo la Mradi wa Bomba la Mafuta akiwamo Magimbi Nagaja, anasema yeye ni miongoni wa watu ambao wamefidiwa kupisha mradi huo na amejengewa nyumba nzuri na sasa anafanya tena kazi za kibarua na kumuingizia kipato.

Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Fedha na Mipango Emmanuel Tutuba akizungumza kwenye kiwanda cha mfumo wa kupasha Joto Mafuta.

Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Nishati Mhandisi Felchesmi Mramba akizungumza kwenye ujenzi wa kiwanda cha Bomba la Mafuta, cha mfumo wa kupasha Joto mafuta.
Mratibu wa Mradi wa Bomba la Mafuta kitaifa kutoka Wizara ya Nishati Kisamarwa Nyang'au, akizungumza kwenye ujenzi wa kiwanda cha Bomba la Mafuta, cha mfumo wa kupasha Joto mafuta.

Kaimu Meneja wa kiwanda cha Mfumo wa kupasha Mafuta Joto Wiliam Kajagi akitoa maelezo ya maendeleo ya ujenzi wa kiwanda hicho.

Mkuu wa wilaya ya Nzega (ACP) Advera Bulimba, akizungumza kwenye ujenzi wa kiwanda hicho cha Bomba la Mafuta.

Mwananchi Magimbi Nagaja akielezea namna walivyolipwa fidia zao kupisha kiwanda hicho cha Bomba la Mafuta, pamoja na kupata kibarua kwenye mradi huo na kujiingizia kipato.

Viongozi wakiendelea na ziara kwenye kiwanda hicho cha Bomba la Mafuta wilayani Nzega.

Viongozi wakiendelea na ziara kwenye kiwanda hicho cha Bomba la Mafuta wilayani Nzega.

Viongozi wakiendelea na ziara kwenye kiwanda hicho cha Bomba la Mafuta wilayani Nzega.

Mitambo ya ujenzi ikiwa eneo la kiwanda cha Bomba la Mafuta.

Kazi ikiendelea kujenga kiwanda hicho cha Bomba la Mafuta.

Muonekano wa Makazi mapya ambayo wananchi wamejengewa nyumba kupisha eneo la ujenzi wa kiwanda hicho cha Bomba la Mafuta.

Muonekano wa Makazi mapya ambayo wananchi wamejengewa nyumba kupisha eneo la ujenzi wa kiwanda hicho cha Bomba la Mafuta.

Viongozi wakipiga picha ya pamoja kwenye eneo la makazi ya wananchi ambao wamejengewa nyumba mpya mara baada ya kupisha mradi wa Bomba la Mafuta.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464