Damian Masyenene, Mwanza
BADO serikali inapambana na changamoto ya akina mama wajawazito kuhudhuria kliniki kwa mara ya kwanza ndani ya wiki 12 za mwanzo wa ujauzito kutokana na wanawake wengi kuendelea kukumbatia mila na dhana potofu zinazosababisha kuwepo kwa vifo vya watoto wachanga kabla na baada ya kujifungua.
Katika hotuba ya bajeti ya wizara ya afya kwa mwaka 2021/2022, Waziri Ummy Mwalimu alisema wajawazito 1,760,707 walihudhuria kliniki katika kipindi cha Julai 2020 hadi Machi 2021 ambao ni zaidi ya tarajio la wajawazito 1,650,000 sawa na ongezeko la asilimia 6.7 waliotegemewa katika kipindi hicho.
Hata hivyo, ni asilimia 36 tu walihudhuria kliniki kwa mara ya kwanza ndani ya wiki 12 za mwanzo wa ujauzito, kiwango hicho kidogo kikichangiwa na mila na desturi za kutotoa taarifa za mimba changa katika kipindi hiki huku akitoa wito kwa wajawazito kuhudhuria kliniki mapema.
“Natoa rai kila mjamzito kuhudhuria kliniki mapema mara tu anapogundua kuwa ni mjamzito ili aweze kupatiwa huduma za uchunguzi wa maendeleo ya ukuaji wa mimba pamoja na kukinga na kuzuia matatizo kama vile upungufu wa damu na dalili kuelekea kifafa cha mimba mambo ambayo ndiyo yanachangia vifo katika kipindi cha ujauzito na uzazi kwa kiasi kikubwa,” alisema Ummy.
Kuendelea kuwepo kwa dhana potofu ya kina mama wajawazito kutotoa taarifa za mimba mapema kumeikutanisha Shinyanga Press Club Blog na Mratibu wa elimu ya afya kwa umma mkoa wa Mwanza, Denis Kashaija ambaye anatoa ufafanuzi wa mambo mbalimbali na umuhimu wa kuhudhuria mapema kliniki.
Kashaija anasema katika maeneo mengi ya mikoa ya Kanda ya Ziwa kina mama wengi wanapopata ujauzito wanasubiri matumbo yaonekane ndipo hujitokeza kuanza mahudhurio kliniki hali ambayo inachangiwa na mila potofu wajawazito wakiamini kuanza mapema kliniki watafikiriwa vibaya na kwamba ujauzito utapotea.
Anafafanua kuwa mjamzito akiwahi kliniki ni faida kwake kwani atapata huduma muhimu za awali ambazo kiumbe kilichomo tumboni mwake kinastahili kuzipata na ni vyema kuwahi pale tu wanapojihisi ni wajawazito.
“Kumekuwa na ongezeko la watoto wachanga kufia tumboni mwa mama zao ambao wanafariki kabla ya kuzaliwa kutokana na mama kuwa na magonjwa ya ngono na kwenye mfumo wake wa uzazi ambayo hayakugundulika mapema, lakini kama angepima miezi ya kwanza na akapata matibabu tunaamini mtoto aliyeko tumboni atakuwa salama,” alisema na kuongeza
“Kutokana na ongezeko hilo la vifo watalaam wanashauri anapojihisi ni mjamzito awahi kwenye kituo cha kutolea huduma kliniki za wajawazito apate vipimo na kuanza huduma muhimu ikiwemo dawa zinazosaidia kuongeza sehemu ya virutubisho katika mwili wake vitakavyoufanya ujauzito uendelee kukua katika hali ya usalama na kufikia umri unaostahili,”.
Katika taarifa ya mafanikio ya wizara ya afya kusherehekea miaka 60 ya uhuru ilibainisha kuwa hadi kufikia Machi 2021 vifo vya watoto wachanga ndani ya siku 28 (neonatal mortality) vimepungua kutoka vifo 32 kwa kila vizazi hai 1000 (2004/05) hadi vifo 20 kwa kila vizazi 1000 (2020) huku vifo vya wajawazito navyo vikipungua kutoka 870 kwa kila vizazi 100,000 (1990) kufikia vifo 321 kwa kila vizazi hai 100,000 (2020)
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464