Mhandisi wa Kiwanda cha Ushirika wa Kilimo na Masoko Chato cha kusindika mafuta ya alizeti (Chato AMCOS Sunflower Oil double refining factory) cha chama cha Msingi cha Ushirika (AMCOS) Chato, Mashaka Missana akionesha mafuta yalisindikwa katika kiwanda hicho.
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Baada ya Vyama Vya Msingi vya Ushirika (AMCO) vilivyokuwa
vimesinzia kufufuliwa na kuanzishwa mpya kwenye mikoa kwenye mikoa inayolima
zao la pamba, nguvu ya Ushirika imeanza kuonekana.
Wakitembelea Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS)
vinavyolima zao la pamba na alizeti wilayani Kishapu mkoani Shinyanga na Chato
mkoani Geita kwa nyakati tofauti mapema wiki hii, Maafisa Mawasiliano wa Wizara
ya Kilimo na Waandishi wa habari wameona nguvu ya Ushirika inavyoweza
kubadilisha mbinu za uzalishaji na kuchangia maendeleo ya uchumi wa mtu mmoja na
nchi kwa ujumla.
Wakiwa katika Chama cha Msingi cha Ushirika (AMCOS) Kishapu mkoani Shinyanga,
wamekutana na Trekta ambayo imenunuliwa na AMCOS hiyo kwa fedha taslimu Milioni
35 ambazo zimetokana na kiasi cha shilingi milioni 15 walizopewa mkopo na Benki
ya NMB kwa riba ya asilimia 9% mkopo ambao watarejesha ndani ya miaka mitatu,
jambo ambalo wamesema liko ndani ya uwezo wao.
“Trekta hili litasaidia kuongeza uzalishaji kwa wanachama
wetu, pia tutawalimia wakulima wengine hivyo tutaongeza uzalishaji wa zao la
pamba na mazao mengine”,alisema Mwenyekiti wa Kishapu AMCOS, Emmanuel Sona.
“Tumefanikiwa pia kudhibiti ubora wa pamba ambapo sasa
wakulima wameachana na tabia ya kuchafua pamba kwa kuongeza mawe, maji na
mchanga na vitu vingine. Tunashukuru bei ya pamba iko vizuri na haijashuka
kwenye bei elekezi ya serikali shilingi 1560 kwa kilo moja ya pamba lakini
tunaomba wanunuzi waje kununua pamba kwa bei ya ushindani”,amesema Sona.
Na huko mkoani Geita ,Chama cha Msingi cha Ushirika (AMCOS) kimeanzisha Kiwanda cha Ushirika wa Kilimo na Masoko Chato cha kusindika mafuta ya alizeti (Chato AMCOS Sunflower Oil double refining factory), wamenunua lori la mizigo, trekta na kujenga ghala la kuhifadhia nafaka kutokana na ushuru walizokusanya na mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB).
“Ununuzi wa zana hizi za kilimo umeongeza uzalishaji na kuwapa wananchi unafuu wa upatikanaji wa mafuta,kulimiwa mashamba na kusomba mizigo pamoja ajira”, alisema Katibu wa Chato AMCOS Daudi Mahelule.