WAFANYABIASHARA WA MPUNGA SHINYANGA WABAINISHA SABABU KUPANDA KWA BEI YA MCHELE

Na Halima Khoya, SHINYANGA

WAFANYABIASHARA wa Mpunga mkoani Shinyanga, wameeleza sababu za kupanda kwa bei ya Mchele, kuwa inatokana na kuadimika kwa zao la Mpunga Sokoni.

Wafanyabiashara wamebainisha hayo leo Julai Mosi 2022 wakati wakizungumza na waandishi wa habari.

Mmoja ya wafanyabiashara hao Juma  Ally, amesema upatikanaji wa mpunga kwa msimu huu ni mchache, kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa iliyopelekea mpunga kuwa kidogo na kusababisha mfumuko wa bei ya Mchele.

Amesema awali walikuwa wakinunua gunia moja la Mpunga Sh.40,000 hadi 45,000, lakini sasa hivi wananunua gunia kwa Sh. 90,000 hadi 102,000, na kusababisha kupanda kwa bei ya Kilo ya Mchele kutoka Sh. 1,200 hadi, 2,000 na kupelekea kupanda kwa gharama za maisha kwa wananchi hasa wa hali ya chini.

Kwa upande wake Mmoja wa Wakulima wa zao la Mpunga Athumani Mashoto, ametoa wito kwa Serikali kuwekeza kwenye mabwawa ili kufanya kilimo cha umwangiliaji na kuacha kutegemea kilimo cha mvua, hali ambayo itasaidia upatikanaji wa chakula kingi na kuondokana na mfumuko wa bei ya vyakula.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464