Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu akikata utepe wa gari kuashiria uzinduzi wa gari baada ya makabidhiano ya gari. Kushoto kwake ni Kiongozi wa Huduma za Kijamii kutoka USAID Tanzania, Dr. Ifeyanwa Udo
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chaula akiendesha gari lililotolewa kwa Wizara hiyo kama ishara ya kulipokea rasmi.
Picha ya magari matatu ambayo yametolewa kwa Ofisi ya Rais TAMISEMI; Wizara za Afya; Wizara ya Maendelo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu.
Shirika la Marekani la Maendelo ya Kimataifa (USAID) kupitia Mradi wa ACHIEVE unaotekelezwa na Shirika la Pact Tanzania limetoa magari matatu kwa Serikali ya Tanzania. Thamani ya magari haya ni Shilingi 236,555,851 za Kitanzania na yametolewa kwa ajili ya kurahisisha utendaji na uratibu wa sera katika huduma za ustawi wa jamii, afya ya jamii na huduma kwa watoto waishio katika mazingira hatarishi katika Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya Afya na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu. Magari yaliyotolewa ni pamoja na Landcruiser Hardtop (2) na Landcruiser Prado (1).
Magari haya yanakusudiwa kutumika na Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Iliyopo katika Ofisi ya Rais TAMISEMI; Idara ya Ustawi wa Jamii iliyopo katika Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu; na Kitengo cha Elimu Afya katika Wizara ya Afya.
Mawaziri, Makatibu wakuu, na Watendaji katika Wizara hizi lengwa wamepongeza juhudi hizi zenye mlengo wa kuimarisha na kutengeneza uratibu endelevu na madhubuti wa utekelezaji wa sera. “Hatua hii ni sehemu ya ndogo tu katika bahari ya mafanikio mengi yanayotokana na ubia kati ya Serikali ya Marekani na Serikali ya Tanzania.
USAID kupitia Mradi wa ACHIEVE imechochea kupatikana kwa matokeo makubwa katika uimarishaji wa mifumo ya huduma za ustawi wa jamii ikiwemo utengenezeaji wa miongozo, na uwezeshaji wa wa utekelezaji wa sera na mikakati mbalimbali,” alisema Dkt. Zainab Chaula, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu.
Katiba hotuba yake, Kiongozi wa Huduma za Kijamii kutoka USAID Tanzania, Ifeyingwa Udo aliasa Serikali ya Tanzania kuendelea kuwekeza na kutenga raslimali kwa ajili ya afua za kimkakati katika utoaji wa huduma za kijamii ili kuwezesha makundi yaliyo katika mazingira hatarishi na yenye kukabiliwa na umaskini kupata huduma stahiki.
“Utengenezaji wa mifumo imara ya utoaji wa huduma za kijamii kwa makundi yaliyo katika mazingira hatarishi ni sehemu ya vipaumbele vya Serikali ya Marekani. Makabidhiano ya Magari haya ni hatua muhimu katika kuhakikisha uratibu wa sera wenye tija katika utekelezaji. Tunaahidi kuendelea kufanya kazi na Serikali ya Tanzania ili kuimarisha mifumo hii muhimu kwa kujengea jamii ustahimilivu na kuwaungisha watu walio katika mazingira hatarishi na huduma kama upimaji wa Virusi vya UKIMWI, matibabu na matunzo kwa watu waishio na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI,” alisema Ifeyinwa.
Tangu mwaka 2020, Mradi wa ACHIEVE umekuwa ukifanya kazi na Serikali ya Tanzania kupitia uwezeshaji wa kitaalamu na hata kifedha. Uwezeshaji huu umetumika kutengenezea sera, miongozo na kutoa mafunzo katika kada za ustawi wa jamii, na afya ya jamii ili kuboreha upatikanaji wa huduma kwa watoto waishio katika mazingira hatarishi, vijana balehe na watu waishio na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI.
Akizungumza wakati wa makabidhiano haya, Mkurugenzi Mkazi wa Pact Tanzania ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mradi wa ACHIEVE, Levina Kikoyo alisema “Mifumo imara ya utoaji wa huduma za ustawi wa jamii huraghabisha kasi na ubora wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Tunafanya kazi ya kuboresha mifumo hii ili kuwezesha ujumuishwaji wa makundi yaliyo katika mazingira hatarishi katika uzalishaji na shughuli nyinginezo za kiuchumi, kuhimili na kutokomeza majanga kama VVU na UKIMWI, na pia kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya. Aidha kupitia kazi hii, tunachochea ushiriki wa wadau wengine kama sekta binafsi na mtu mmoja mmjoa kushiriki katika kuimarisha huduma za ustawi na afya ya jamii.”
ACHIEVE ni mradi wa miaka mitano (2019-2024) unaotekelezwa katika nchi tisa duniani. Mradi huu unafadhiliwa na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID). Kwa Tanzania, ACHIEVE ni mradi wa miaka minne (2020-2024) unaolenga katika kuboresha huduma za kukabiliana na Virusi vya UKIMWI (VVU) miongoni mwa watoto waishio katika mazingira hatarishi. Kufikia lengo hili, Mradi wa ACHIEVE unatoa huduma kwa watoto waishio katika mazingira hatarishi na kutekeleza afua ya DREAMS.
Pia, Mradi wa ACHIEVE umelenga kuboresha mifumo ya huduma za ustawi wa jamii ili kuboresha ubora na upatikanaji wa huduma hizo. Vilevile, Mradi wa ACHIEVE unajengea uwezo na kuzisaidia AZAKI za wazawa kuwa na mifumo rasmi na imara ya kiutendaji kwa ajili ya huduma endelevu katika ngazi ya jamii. Mradi wa ACHIEVE unatekelezwa katika Halmashauri 95 zilizopo katika Mikoa 26 ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.
Mradi wa ACHIEVE unatekelezwa na Shirika la Pact kama Shirika Kiongozi kwa ubia na mashirika ya Palladium, No Means No, na WI-HER. Wabia hawa wanatekeleza mradi wa kusaidiana na AZAKI za wazawa.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464