DIWANI AWATAKA WANANCHI WACHANGAMKIE FURSA YA MIKOPO YA HALMASHAURI KUJIKWAMUA KIUCHUMI


 
Diwani wa Ngokolo Victor Mkwizu, akizungumza kwenye mkutano.

Wananchi wakiwa kwenye mkutano.

Wananchi wakiwa kwenye mkutano.

Na Suzy Luhende, SHINYANGA

Diwani wa kata ya Ngokolo Manispaa ya Shinyanga Victor Mkwizu, amewataka wananchi wa kata hiyo kuchangamkia fursa ya mikopo inayotolewa na Halmashauri ya manispa ya Shinyanga asilimia 10 na kujikwamua kiuchumi.


Amebainisha hayo leo Agosti 23, 2022 wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Ngokolo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika mtaa wa Kalonga kata ya Ngokolo manispaa ya Shinyanga, ambapo amewataka wananchi wote wachangamkie fursa ya mikopo hiyo , ambayo asilimia Nne hutolewa kwa vijana na wanawake na asilimia mbili kwa watu wenye ulemavu.


Victor amewaomba wafuate utaratibu unaotakiwa wafike kwenye ofisi ya mtendaji wakapate utaratibu ili waweze kupatiwa mikopo waweze kujikwamua kiuchumi na kufanya maendeleo katika kata ya Ngokolo.


"Niweze kuwahamasisha kina mama vijana na watu wenye ulemavu ndani ya kata yangu hii, muweze kuichangamkia fursa hii, mimi kazi yangu mkiwa tayari mtanitaarifu nitasimamia manispaa ili muweze kupewa mikopo hiyo kwa wakati, muweze kujishughulisha na biashara mbalimbali na kujikwamua kiuchumi"amesema Mkwizu


Pia amezungumzia soko la Ngokolo mitumbani, amesema tayari ameshaongea na mkurugenzi wa manispaa kwa ajili ya kutengenezewa miundombinu ya soko hilo, ili liwe soko kuu la Ngokolo, tayari wamekubaliana litajengwa ili wananchi wa Ngokolo wafaidike na kuweza kufanya maendeleo na kujiongezea uchumi.


"Hoja hii tayari nimeshaipeleka manispaa na mkurugenzi amekubali ila alikuwa anamalizia kukarabati stendi ndogo ya mjini, amesema akimaliza atashughulikia soko letu hivyo wananchi wa Ngokolo tukae mkao wa kula"amesema.


Baadhi ya wananchi walisema kero zilizopo mitaani kwao, Moshi Charles mkazi wa mtaa wa mageuzi amesema barabara ya Mageuzi haina Kalvati, hivyo mvua ikinyesha maji yanatuama yanajaa hadi mlangoni yanakuwa hayatembei na barabara haina molamu, amemuomba diwani alifikishe sehemu husika ili liweze kutatuliwa, kwani imekuwa kero kubwa.


Kwa upande wake mwenyekiti wa mtaa wa Mageuzi Erick Elias amesema kweli mwananchi wake ameuliza swali sahihi kwani hiyo ni barabara ya Mageuzi ambayo imepewa jina la Emma Sanga ni barabara kuu ya kuelekea Dodoma imekuwa ni kero na si kalvati moja inahitaji kalvati mbili ili ikae sawa, walishafika Tarura kuiona wakaahidi wataifanyia kazi.

Theresia Mwegeso mkazi wa mtaa wa Mwadui amesema taarifa iliyosomwa na mtendaji imesema kuna sh 150 milioni imetolewa kwenye vikundi vya wajasiliamali Ngokolo lakini kuna shida kubwa sana kina mama wanahangaika na kwenye vikundi vya wakopeshaji na wengine wamenyang'anywa mali zao, sijui hilo unalifahamu, na kuna vikundi Ngokolo vimepewa fedha za manispaa.

"Mheshimiwa diwani tumesikia kwenye taarifa ya mtendaji imesema sh 150 milioni, umehakiki kweli hivyo vikundi vimetoka Ngokolo isije kuwa vikawa vikundi vingine vimetumia jina la Ngokolo, maana nimefatilia hakuna hata kikundi ninachokijua cha Ngokolo kama kuna kundi hata moja tu lingesimama lakini tuna amini hakuna"amesema Mwegeso.

"Hatuna eneo rasmi kwa ajili ya wajasiliamali tunaomba litengwe eneo la soko kama maeneo mengine ili tunufaike nasisi, kwani tunapokuwa na mahitaji ya kununua vitu mbalimbali kama mboga mboga inatubidi tutumie usafiri kwenda kata zingine ambako kuna masoko na tunatembee mwendo mrefu kwa ajili ya kupata mahitaji yetu, hivyo tunaomba hilo lifanyiwe kazi"amesema Mwegeso.

"Pia amesema barabara ya kuingia shule ya msingi Ngokolo haipitiki wakati wa mvua inakuwa na tope sana, hivyo mtoto ili avuke kuelekea shuleni lazima avue viatu, tunaomba barabara iwekewe moramu ili watoto wetu wanapopita wapite kiurahisi"pia tunaomba litengwe eneo la soko katika mtaa wetu wa Mwadui'ameongeza.

Hata hivyo wananchi wa kata ya Ngokolo wamesema kero nyingi ambazo diwani wa kata hiyo Victor Mkwizu aliahidi atazishughulikia na atazipeleka sehemu husika ili zikafanyiwe kazi kwa wakati ili wananchi wa kata hiyo waweze kufanya kazi zao za kimaendeleo, pia aliwaomba kuwa na umoja na ushirikiano pale watakapokuwa na tatizo wamtaalifu ili aweze kutatua kwa wakati.


"Kata yetu ni kubwa ina mitaa saba ni kata kubwa kuliko kata zote hapa manispaa na ina watu wengi, lakini tukishirikiana kwa pamoja tutafanya mambo makubwa ya kimaendeleo, hivyo cha muhimu naomba tujitokeze wote ili tuhesabiwa kwa ajili ya kupata maendeleo zaidi"amesema Victor.





Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464