MZEE WA MIAKA 70 AKATAA FIDIA YA SH MILLIONI 20 ALIYOPEWA KWAAJILI YA FIDIA YA ARDHI.


Mzee Munuo akiwa kwenye shamba lake katika kitongoji ya Nyangaka.


Na . Patrick Mabula ,

MKAZI wa kijiji cha Kakola halmashauri ya Msalala wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga Benson Munuo (70) amegoma malipo ya shilingi Millioni 20 kama fidia ya ardhi ya shamba lake lenye ukubwa wa ekari 15 akidai limepimwa viwanja bila yeye kuhusishwa.



Akiongea na waandishi wa habari kijijini hapo juzi mzee Munuo ameilalamikia halmashauri ya Msalala kwa kitendo cha kulipima viwanja vya makazi shamba lake pasipo yeye kushirikishwa wala makubaliano yeyote hali iliyofanya agome kupokea kiasi hicho.

"Shamba langu lililopo kitongoji cha Nyangaka kata ya Bugarama limepimwa viwanja vya makazi wakati nilishaliendeleza na lina rasilimali ambazo ni mabwawa matatu anayofuga samaki , miti mbalimbali ya mbao na matunda zaidi 1000 , mazao ya chakula , migomba, mihogo, miwa, mitikiti , mapalachichi , katani na mizinga ya nyuki pia ninafuga."amesema Munuo.

Mzee Munuo amesema upimaji uliofanywa wa viwanja vya makazi na kupandwa alama ya vigingi hautambui kwa sababu hakushirikishwa na amegoma kupokea pesa za fidia kwa sababu hazilingani na thamani ya mali zake alizowekeza katika shamba lake na kuomba taratibu zifuatwe kwa mjibu wa sheria ya ardhi.

Jirani yake Issa Ibrahim amesema eneo hilo aliloliendeleza kwa miaka 11 alilinunua mwaka 2007 baada ya kustaafu kazi katika mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu na kuamua kuwekeza hapo kwa shughuli zake za kilimo cha mazao mbalimbali .

Mtema Nkamba jirani yake amesema Munuo hajawahi kushirikishwa juu ya upimaji wa shamba lake na toka lipimwe watu wasiofahamika wamelivamia na kuanza kuvuna miti na mazao yake ya chakula pamoja na kuchoma moto eneo hilo na kumsababishia hasara kubwa ya mali zake zilizopo hapo.

Mwenyekiti wa Serikali wa kitongoji cha Nyangaka , Pili Msomi alipoulizwa amesema kabla ya upimaji huo kufanyika walihitisha mkutano wa hadhara juu ya suala hilo lakini mzee Munuo hakuweza kuhudhulia kwenye kikao hicho hali iliyozusha malalamiko hayo baada ya halmashauri kufanya kazi hiyo.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Msalala Charles Fussi alipoulizwa alikiri kuwepo kwa upimaji wa maeneo mbalimbali katika halmashauri yake baada ya serikali kuwapatia kiasi cha shilingi Billioni 1.6 kwa ajili ya kazi hiyo pamoja na kulipa fidia na kuwataka kwa yeyote mwenye malalamiko kufika ofisini . Mzee Munuo akiwa kwenye shamba lake katika kitongoji ya Nyangaka.
Mzee Munuo akiwa kwenye shamba lake akionyesha baada ya kukataa fidia.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464