SITA MBARONI WAKITOROSHA MADINI YA DHAHABU, WADAKWA NA MABURUNGUTU YA FEDHA


Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Janeth Magomi akionesha fedha na madini ya dhahabu ambayo wameyakamata yakitoroshwa.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Janeth Magomi akionesha fedha na madini ya dhahabu ambayo wameyakamata yakitoroshwa.
Maburungutu ya fedha ambazo zimekamatwa wakiwanazo watuhumiwa hao.
 
Na Marco Maduhu, SHINYANGA

JESHI la Polisi mkoani Shinyanga, limewakamata watu Sita wakitorosha Madini ya dhahabu katika barabara ya Ilogi wilayani Kahama mkoani Shinyanga.

Watu hao wamekamatwa wakiwa na Madini ya dhahabu yenye uzito wa Gramu 930.88 yenye thamani ya Sh.milioni 93, huku wakiwa na fedha Taslimu kwenye begi Sh. milioni 97.02.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Janeth Magomi amebainisha hayo leo Agosti 11, 2022 wakati akizungumza na waandishi wa habari, amesema kuwa watu hao walikamatwa jana majira ya saa tatu usiku.

Amesema Askari Polisi wakiwa katika doria ya kawaida, waliwasimamisha watu hao sita wakiwa na gari aina ya Toyota yenye namba T.913 DRX katika barabara hiyo ya Ilogi kuelekea mkoani Geita, ndipo wakawakuta na Madini hayo pamoja na fedha hizo kwenye begi.

"Wakati wa upekuzi wa gari hilo tulifanikiwa kukuta Madini ya dhahabu yenye uzito wa Gramu 930.88 yenye thamani ya Sh. milioni 93, Pesa Taslimu Sh. milioni 97, Mzani Mmoja wa kielektroniki wa kupimia dhahabu pamoja na mashine Moja ya kupima ubora wa dhahabu,”amesema Magomi.

“Uchunguzi wa awali unaonesha kuwa watuhumiwa walikuwa wakitorosha madini haya kwenda nje ya nchi kwa lengo la kukwepa kulipa kodi na tozo za Serikali, kitendo ambacho ni kosa kisheria,” ameongeza.

Aidha, amesema taratibu za kipolisi zinaendelea kufanyika, na zitakapokamilika watuhumiwa watafikishwa Mahakamani, huku akitoa wito kwa wananchi hasa wanaojihusisha na biashara za madini wafuate taratibu zote za kisheria.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464