TANROADS SHINYANGA YAWATAKA WANANCHI KUHESHIMU MAENEO YA HIFADHI ZA BARABARA, WANANCHI NA WAO WAHOJI FIDIA YA MAENEO YAO
Meneja Tanroads Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Mibara Ndirimbi akizungumza na waandishi wa habari (hawako pichani) kuhusu mikutano ya mafunzo kwa wananchi inayoendeshwa na Ofisi yake.
Msimamizi wa Kitengo cha matengenezo - Tanroads mkoani Shinyanga, Mhandisi Ferdinand Mdoe akitoa elimu ya matumizi sahihi kwa wakazi wa kijiji cha Mawemilu kata ya Mwakitolyo wilayani Shinyanga.
Mmoja wa wakazi wa kijiji cha Mawemilu, Kayoloo Mwanamajige akiuliza swali kuhusu upitishaji wa mifugo katikati ya barabara mbele ya watendaji wa Tanroads mkoani Shinyanga.
Wakazi wa kijiji cha Mawemilu, kata ya Mwakitolyo Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wakifuatilia mkutano uliofanyika kwenye kijiji chao kwa ajili ya kuzungumzia matumizi sahihi ya Hifadhi ya barabara.
Na Suleiman Abeid
WAKALA wa barabara nchini (TANROADS) mkoani Shinyanga umewataka watu wote waliojenga nyumba za makazi ama kwa ajili ya shughuli za kibiashara kwenye maeneo ya hifadhi ya barabara kubomoa nyumba zao kuanzia sas na waache wazi maeneo hayo kama sheria za barabara zinavyoelekeza.
Agizo hilo limetolewa Meneja Tanroads mkoani Shinyanga, Mhandisi Mibara Ndirimbi wakati akitoa elimu ya matumizi bora ya barabara kwa wananchi wanaoishi kandokando ya barabara pamoja na madereva wa magari makubwa.
Mhandisi Ndirimbi amesema mtu ye yote anayejenga nyumba ya makazi ama kuendesha shughuli zozote za kibiashara ndani ya maeneo ya hifadhi ya barabara anakuwa amevunja sheria na anastahili kuchukuliwa hatua.
Kutokana na hali hiyo Mhandisi Ndirimbi ameagaiza kubomolewa kwa nyumba zote zilizomo ndani ya hifadhi ya barabara huku akisisitiza madereva wa magari yanayosafirisha mizigo kuhakikisha wanabeba mizigo kulingana na uzito wa gari husika.
Amesema maeneo ya hifadhi ya barabara hutengwa kwa madhumuni mbalimbali ikiwemo shughuli za dharura zinazoweza kujitokeza kwenye magari yanayotumia barabara hizo na madereva kulazimika kuegesha magari pembeni kwa ajili ya matengenezo.
“Leo hii tumefanya mikutano mitatu, tumefanya hapa Kahama mjini kwenye eneo la maegesho ya magari makubwa yanayoenda nchi za nje, pale Tinde kwenye mizani ya kupimia magari na kule kata ya Mwakitolyo katika kijiji cha Mawemilu ambako tumetoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya barabara,”
“Na matumizi sahihi ya barabara tunapozungumza ni juu ya kulinda barabara zetu zisiharibike kabla ya muda wake uliopangwa wa kutumika ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wasafirishaji wanabeba uzito unaokubalika kwa mujibu wa sheria ya 2016 ya Afrika Mashariki inayotaka magari kubeba uzito unaokubalika,” anaeleza Mhandisi Ndirimbi.
Amesema lengo kubwa ya kuendesha mikutano hiyo ni kuwawezesha wananchi wawe na uelewa wa kutosha na wasiingie kwenye kutenda makosa ambayo hawayaelewi na kwamba mikutano hiyo imewashirikisha wananchi wengi ikiwemo watendaji wa Serikali, TAKUKURU na Jeshi la Polisi.
Mhandisi Ndirimbi ametoa wito kwa wananchi wote ambao wamejenga nyumba za makazi katika maeneo ya hifadhi ya barabara kuanza utaratibu wa wao wenyewe kubomoa majengo yao na vibanda ambavyo vimejengwa ndani ya hifadhi hizo kabla ya hatua zaidi kuchukuliwa dhidi yao.
“Wiki ijayo kuanzia Jumatatu (Septemba 5, 2022) tutatoa notisi ya siku zisizopungua thelathini kwa wale wote waliomo ndani ya hifadhi za barabara kuwa wameondoka ndani ya maeneo hayo kwa hiari yao wao wenyewe bila kusukumwa ili maeneo ya hifadhi yawe salama,” anaeleza Mhandisi Ndirimbi.
Wakati huohuo wakazi wa kijiji cha Mawemilu kata ya Mwakitolyo wilayani Shinyanga wameomba kuelimishwa juu ya utaratibu wa ulipwaji fidia kwa wale watakaobomoa ama kubomolewa nyumba zao zilizomo ndani ya hifadhi ya barabara.
Baadhi ya wananchi hao wamedai kukutwa na barabara na kwamba taarifa za wao kuvamia maeneo hayo siyo za kweli ambapo wameomba Serikali iwatendee haki kwa kuwalipa fidia ili waweze kuhama na kupisha maeneo ya hifadhi ya barabara.
Kwa upande wao Kabisi Lusanika na Kayoloo Mwanamajige wamehoji suala la upitishaji wa mifugo ndani ya barabara kwamba watumie utaratibu upi wa kuvusha ng’ombe zao kutoka upande mmoja wa barabara na kwenda upande wa pili ili wasivunje sheria.
“Hapa mmetueleza tusipitishe mifugo barabarani, na kwamba barabara yetu hapa hivi karibuni itajengwa kwa kiwango cha lami, je sisi tunaotaka kupitisha ng’ombe kutoka upande mmoja kwenda upande wa pili tufanyeje ili tusivunje sheria?” anahoji Lusanika Shija.
Katika majibu yake ya jumla kwa wananchi wa kijiji cha Mawemilu, mmoja wa watendaji wa Tanroads mkoani Shinyanga, Renatus Kulwa amesema suala la upitishaji wa ng’ombe barabarani kuna utaratibu umewekwa wa kuwasaidia wafugaji ili ng’ombe wao wasiathiri barabara.
“Kama kuna eneo lina mifugo tayari sheria zetu zinaagiza pawekwe alama itakayoonesha eneo hilo ni njia ya kupitishia mifugo, hivyo iwapo barabara hii itawekewe lami, patakuwa na maeneo maalumu yenye alama kwa ajili ya kuvukishia mifugo yenu,”
“Hata kwenye hizi barabara zetu za vumbi tayari yapo maeneo maalumu yametengwa kwa ajili ya kuvushia mifugo, hata kwenye barabara zote kubwa yapo maeneo maalumu yametengwa na yamewekewa alama ya ng’ombe, na kama hayapo, basi meneja Tanroads ataweka alama hizo,” anaeleza Renatus Kulwa.
Kwa upande wake Msimamizi wa kitengo cha matengenezo ya barabara Tanroads mkoani Shinyanga, Mhandisi Ferdinand Mdoe ametoa wito kwa wakazi wote wa kijiji cha Mawemilu ambao wamejenga nyumba ndani ya hifadhi ya barabara waondoe majengo yao na waheshimu sheria za barabara.
“Sheria zetu za barabara ziko wazi, mtu ye yote haruhusiwi kujenga ndani ya hifadhi ya barabara, na hii ni ndani ya mita thelathini kila upande kuanzia katikati ya barabara, hivyo ye yote aliyemo ndani ya hifadhi aondoke kwa hiari bila kushurutishwa,”
“Kuhusu malipo ya fidia hii itatolewa kwa wale watakaobainika walikuwa ndani ya maeneo hayo ndani ya kipindi cha miaka ya zamani 1936 hadi Juni, 2007 hawa watafanyiwa utaratibu wa kulipwa fidia zao, lengo letu kwa sasa ni kutoa elimu ili kila mtu aelewe juu ya umuhimu wa utunzaji wa hifadhi za barabara zetu,” anaeleza Mhandisi Mdoe.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464