Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Shinyanga Mjini, Abubakar GulamHafiz Mukadam akizungumza na waandishi wa habari Mjini Shinyanga leo
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Shinyanga Mjini, Abubakar GulamHafiz Mukadam amewataka Wanachama wa CCM kujitokeza kwa wingi na kushiriki kikamilifu katika Mkutano Maalumu wa Uchaguzi wa Nafasi ya Uenyekiti wilaya huku akiwasihi wale waliokuwa na upendo na mategemeo ya kumchagua tena kuwa mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini wapokee maamuzi ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) ambayo imewateua Mokhe Warioba Nassor, Magile Anold Makombe na Pendo John Sawa kugombea nafasi hiyo.
Abubakar GulamHafiz Mukadam ni miongoni mwa Makada wa CCM waliokuwa wametia nia kugombea nafasi ya uenyekiti CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini akitetea nafasi yake aliyoitumikia tangu mwaka 2017 lakini jina lake halijarudi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamis Septemba 29,2022 Mjini Shinyanga, Abubakar GulamHafiz amesema amepokea kwa moyo mweupe maamuzi ya kikao cha mwisho cha uteuzi cha Halmashauri kuu ya Taifa (NEC) ambacho kinaongozwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akieleza kuwa ni utaratibu wa kawaida katika kutoa uteuzi.
“Binafsi nimelipokea kwa moyo mweupe na kwa nafsi iliyofunguka kabisa kwamba ni jambo la msingi na ni maamuzi ya Mwenyezi kutokupata uteuzi, saa zingine inakuwa ni heri, unaweza kuliona jambo linalotolewa kwamba limetokea jambo baya kwangu kwanini limefanyika kwangu lakini siyo jambo unalolihitaji na linapotokea kuwa vinginevyo ukawa unahisi kwanini limetokea kwako”,amesema Abubakar.
“Kwa hiyo uwepo wa jina au kutokuwepo kwa jina langu ni kikao ndicho kinachoamua, na mimi kama mwanachama ambaye nilitamani kugombea nafasi ya uenyekiti CCM wilaya ya Shinyanga Mjini na niliyetamani kuendelea kutetea nafasi hiyo ninapaswa na sina budi kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu lakini kuheshimu na kutii utaratibu wa vikao na maamuzi yaliyotokea katika vikao vya juu ambavyo ndivyo vinavyotoa uteuzi wa nafasi hizo”,amesema Abubakar.
“Natoa wito kwa wanachama wenzangu wa CCM na hasa waliokuwa na upendo na mategemeo na mimi kwamba wataenda kunichagua tena kuwa mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini wapokee maamuzi hayo.
Tunapaswa na tunawajibika kuheshimu na bila kuwa na manung’uniko, masononeko wala fikra potofu zozote zile. Ni jambo la msingi wanachama na viongozi wote wakawa watulivu na tukaenda kuendelea kutimiza wajibu wetu kwenye Mkutano maalumu wa uchaguzi kuchagua mwenyekiti wa wilaya ambaye Mwenyezi Mungu amemwandaa kuwa mwenyekiti wetu”,ameeleza Abubabar.
Ametoa wito kwa wanachama wenzake wa CCM wilaya ya Shinyanga Mjini na haswa ambao walikuwa na matamanio na shauku ya kwenda kumchagua tena kuwa mwenyekiti kwamba sasa maamuzi ya vikao yamewateua wagombea watatu ambao wataenda kuwachagua ambaye Mwenyezi Mungu ndiye aliyemwandaa mmoja wao.
Amebainisha kuwa kama Mwanachama wa CCM anayeheshimu maamuzi ya vikao ataendelea kuwa mwanachama , mtetezi na mzalendo na mtiifu katika Chama Cha Mapinduzi kwa sababu kimemkuza, kimemlea na kimempa umaarufu katika kipindi chote cha uongozi hivyo ataendelea kukiheshimu na kukithamini na kupokea maamuzi sahihi ya chama.
“Mimi kama mwanachama na kiongozi ambaye nimekuzwa na Chama cha Mapinduzi, nimetengenezwa na Chama cha Mapinduzi na nimekuwa sasa ndani ya uongozi kama miaka 15 kwa mfululizo kwa nafasi mbalimbali. Nimeingia kwenye uongozi wa CCM wa wilaya Agosti mwaka 2017 na ukomo wangu utakuwa Oktoba 1,2022 siku ya mkutano maalumu wa CCM Wilaya siku ambayo tutafanya uchaguzi.
Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kila hatua zinazofanyika ndani ya chama na kwa kipindi chote cha uongozi wangu tangu mwaka 2017 mpaka mwaka 2022”,amesema.
“Na kwa utaratibu wa Chama cha Mapinduzi kwa sisi wanachama wa Chama cha Mapinduzi na haswa ambao tumetokea kuanzia kwenye Greenguard kuja kwenye nafasi mbalimbali za uongozi ikiwemo UVCCM ambako ndiko tunakopikwa, tunaandaliwa uongozi, tunapopewa maadili na kutengenezwa kuwa viongozi tunapaswa kuheshimu misingi, katiba na kanuni na utaratibu ulio wa msingi kabisa ndani ya CCM”,ameeleza.
Amesema hakuna aliye juu ya CCM na kwamba binadamu wana matamanio lakini kila jambo linapangwa na Mwenyezi Mungu, na kwa sababu linapangwa na Mwenyezi Mungu hakuna sababu yoyote ya kuendelea kuwa na manung’uniko.
“Tunapokuwa katika kipindi hiki ambacho nafasi za uongozi zilitangazwa, mimi kama mwenyekiti ninayemaliza muda wangu wa uongozi,niliomba nafasi ya kugombea nafasi ya Uenyekiti wilaya ili kutetea nafasi yangu. Nilitamani kuendelea kuwa mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, niendelee kukitumikia chama kama kiongozi wa CCM”,amesema.
“Mimi Abubakar GulamHafiz Mukadam ni nani ndani ya CCM? . Hakuna aliye juu ya CCM na kwa sababu ndiyo utaratibu huo, sasa kila mmoja ninamuasa ajitahidi kushiriki kwenye mkutano wa uchaguzi, na kwa kuwa mimi bado ni mwenyekiti ninaendelea kuwahamasisha wanachama na viongozi wote ambao ni wajumbe wa mkutano ule waweze kushiriki kwa wingi na kikamilifu, kwa heshima na utiifu ili kutimiza wajibu ambao tunapaswa kufanya”,amesema.
Akifafanua zaidi amesema : “Kwa utaratibu wa CCM,mnapochukua nafasi zile kugombea, mnakuwa mmetia nia na utaratibu wake mtaanza kuwa na vikao kuanzia ngazi wilaya kwa wagombea wa ngazi ya wilaya,kutakuwa na Sekretarieti,usalama na maadili,kamati ya siasa. Na kwa nafasi hizi kubwa Uenyekiti na Uenezi zinatoka kwenye vikao vya wilaya, vinaenda kujadiliwa ngazi ya mkoa, kwa hiyo nafasi yangu baada ya kumaliza kujadiliwa kwenye nafasi ya wilaya inapanda kwenye Sekretarieti,usalama na maadili ngazi ya mkoa, kamati ya siasa na mapendekezo yanapotoka hapo hayaendi tena kwenye halmashauri ya Mkoa, yakitoka hapa yanaenda ngazi ya taifa na taifa kule kunakuwa na vikao vingine”.
“Lakini kwa namna mimi ninavyolielewa binadamu unaweza kuwa na matamanio yako lakini Mwenyezi Mungu kwa matakwa yake anaweza kukuletea jambo ambalo wewe binafsi kwa muonekano wako utaliona kama linaenda vinginevyo lakini Mwenyezi Mungu ambaye kakutengenezea hivyo anafahamu mwisho unakuwa ni mzuri, ni kama heri kwangu kutokupata uteuzi huo lakini pia ni heri kwa wale Mwenyezi Mungu amewajaalia vikao vikaona kwamba ni wanachama sahihi kwa kugombea nafasi hiyo ya uenyekiti wilaya”,amesema.
Septemba 27,2022 NEC ilifanya uteuzi wa majina ya wagombea wa nafasi ya uenyekiti wa CCM wilaya nchi nzima ambapo katika Wilaya ya Shinyanga Mjini walioteuliwa kugombea ni Mokhe Warioba Nassor, Magile Anold Makombe na Pendo John Sawa.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464