Ajali hiyo imetokea leo Jumamosi Septemba 3,2022 majira ya Saa 8 usiku, ikihusisha basi Kampuni ya Super Najimunisa yenye namba za usajili T.413 DAY likitokea Dar es salaam kuelekea Jijini Mwanza, na Fuso yenye namba za usajili T.123 DJH likitokea Mwanza kwenda Dar es salaam likiwa na mzigo wa dagaa.
Manusura wa ajali hiyo Fred Mahina, amesema dereva wa basi hilo alikuwa akiendesha mwendokasi na walipokuwa wakimzuia aliwajibu wangetaka usafiri wa raha wangepanda ndege, huku akiwaambia wasali sana ili wafike salama.
"Tulipofika Morogoro dereva akiwa mwendokasi alikwaruza Roli tukapona kuanguka, lakini akazidi kuendesha mwendokasi abiria tulipokuwa tukipiga kelele apunguze mwendo, aligoma na kutuambia tusali ,ndipo tulipofika hapa Shinyanga na kupata ajali," anasema Mahina.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Leonard Nyandahu ambaye alikuwa eneo la ajali hiyo, amesema chanzo ni uzembe wa Dereva wa basi kwa kutozingatia vibao vya usalama Barabarani na kuendesha mwendokasi.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa mkoa wa Shinyanga Dk. Luzila John amethibitisha kupokea Vifo vya watu watano pamoja na majeruhi 54 ambao wanaendelea na matibabu.
Amesema watu hao ambao wamepoteza maisha bado hawajatambuliwa majina yao, na wamehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti Hospitalini hapo.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464