DC SHINYANGA AZINDUA CHANJO YA POLIO, WATOTO 44,013 WA MANISPAA YA SHINYANGA KUFIKIWA,VIONGOZI WA MITAA WATOE USHIRIKIANO
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akiwa kwenye uzinduzi wa kuchanja watoto chanjo ya polio
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akiwa kwenye picha ya pamoja na watoto baada ya kuzinduwa kwa kuwachanja chanjo ya polio.
Mwenyekiti wa kamati ya afya katika zahanati ya Chamaguha Noera Irege akizungumza juu ya chanjo hiyo.
Mkuu wawaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akiwa na timu ya wataalamu ambao wanapita nyumba kwa nyumba kwa ajili ya kuchanja watoto walio chini ya miaka nitano.
Suzy Butondo, Shinyanga
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko amezindua rasmi kampeni ya chanjo ya matone ya polio nyumba kwa nyumba kwa ajili ya kuwakinga watoto waliochini ya umri wa miaka mitano, ambapo amewataka watendaji na wenyeviti watoe ushirikiano kwa wataalamu wanaofanya kazi ya uchanjaji.
Uzinduzi huo umefanyika leo 1,9,2022 kata ya Chamaguha katika zahanati ya kata hiyo manispaa ya Shinyanga, ambapo amewataka watendaji na wenyeviti watoe ushirikiano kwa wataalamu ili watoto wote walio chini ya umri wa miaka mitano waweze kupatiwa chanjo ya polio.
"Leo tumefanya uzinduzi na tumekuta wazazi wamewaandaa watoto, hivyo tunawaomba wazazi na walezi wengine ambao bado hawajafikiwa wajitokeze kuwatoa watoto wao ili waweze kuchanja tunaanza leo tarehe moja tunamaliza tarehe nne chanjo hii ni kwa ajili ya kuwakinga watoto na ugonjwa usiotibika polio "amesema Mboneko.
Mganga mkuu wa manispaa ya Shinyanga Dkt. Elisha Robert amesema tangu walivyoanza kuchanja mwitikio wa wazazi ni mzuri wamejitokeza kwa wingi na kwa manispaa yote wanategemea kuchanja watoto 44,013.
"Hii chanjo ni mwendelezo hata ukiwa na mtoto amechanjwa wiki mbili moja haina madhara yoyote wasiwe na hofu wazazi, na hili zoezi ni la kitaifa, hivyo watu wote wajitokeze" amesema Dkt.Robert.
Mwenyekiti wa kamati ya afya katika zahanati ya Chamaguha Noera Irege amesema zoezi la chanjo ya polio linaendelea kama kawaida, hivyo anawaomba watu wote wenye watoto walengwa wajitokeze ili waweze kupewa chanjo ya matone watoto wao.
Naye mwenyekiti wa mtaa wa Chamaguha Moshi Ngoyeji amesema wananchi wake wote amewahamasisha, hivyo zoezi litaendelea kama kawaida wazazi wanaendelea kuwatoa watoto kwa ajili ya kuchanjwa.