Na Suzy Luhende,Shinyanga Press Club Blog
Hatimaye wananchi wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga wameanza kunufaika na mgodi wa Almasi wa Williamson Diamond (WDL) kwa kuanza kulipwa sh 1.2 bilioni sawa na asilimia 0.7 ambapo tangu kuanzishwa kwake miaka zaidi ya 80 iliyopita hawakuweza kunufaika na mgodi huo.
Hayo yameelezwa kwenye hafla ya kusaini mkataba kati ya halmashauri ya Kishapu na mgodi wa almas Mwadui, katika ukumbi wa halmashauri hiyo ambapo wamesema toka mgodi huo uanzishwe wananchi walikuwa wananufaika kidogo na mgodi huo.
Akizungumza baada ya kusaini mkataba huo mkurugenzi wa halmashauri ya Kishapu Emmanuel Jonson amesema mwaka 2019 /2020 kulikuwa na changamoto kwenye mgodi huo na kusitisha uzalisha lakini mwaka 2021/2022 mgodi ulikuwa ukitoa Sh milioni 156 ambazo utekelezaji wake haukufanyika kwa sababu uzalishaji wake ulianza mwezi wa 11.
"Mabadiliko haya yataleta maendeleo kwa wananchi kwani fedha hizi zitanufaisha kata tano na vijiji 19 vinavyozunguka mgodi na kutakuwa na miradi ya aina tatu kuanzia ngazi ya vijiji,Kata na miradi itakayosimamiwa na Wilaya ili kuwaondolea changamoto wananchi”amesema Mkurugenzi Jonson.
Amesema kupitia majadiliano waliyofanya na uongozi wa mgodi yamezaa matunda baada ya kusaini mkataba wa Sh bilioni 1.2 sawa na asilimia 0.7 fedha ambayo itakwenda kutekeleza miradi ya maendeleo kwa Kata zinazozunguka mgodi ili ziweze kunufaika.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Kishapu Joseph Mkude amesema jukumu lake ni kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo, hivyo amemtaka meneja wa mgodi huo makubaliano hayo wayatekeleze kwa wakati ,huku akitoa maagizo kwa madiwani wa Kata tano zinazozunguka mgodi kwenda kusimamia miradi itakayotekelezwa kwenye maeneo yao.
"Miradi hii itekelezwe kwa uaminifu na ikaonekane kwenye jamii, mkurugenzi na wakuu wa idara simamieni vizuri ili miradi hiyo iwe ya kiwango, na miradi ya kimkakati mliyonayo nawaomba ikaonekane kwa wananchi ili waweze kunufaika kwa muda mrefu"amesema Mkude.
Meneja mahusiano ya jamii kutoka mgodi wa Williamson Diamond Bernard Mihayo,amesema fedha hizo zikatumike kwa malengo yaliyokusudiwa kwa kutekeleza miradi ya kijamii ambayo iliibuliwa na wananchi na si kwa matumizi mengine ambayo hayakupangwa.
Mwanasheria wa mgodi huo Sylvia Leonidas amesema
mkataba huo ni baina ya Williamson na halmashauri ya Kishapu na wametengeneza
mkataba kwa kuzingatia misingi ya kisheria ya sheria ya madini ya mwaka
2010 toleo la 2019 kipengele cha 105 ambacho kilifanyiwa marekebisho mwaka
2017.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464