TANESCO MKOA WA SHINYANGA YATOA ELIMU KWA WANANCHI WA MWAKITOLYO UOMBAJI WA UMEME KWA NJIA YA NIKONEKTI




Meneja wa Shirika la TANESCO Mkoani Shinyanga, Mhandisi Grace Ntungi akitoa mada kwa wakazi wa kata ya Mwakitolyo wilayani Shinyanga kuhusu utaratibu mpya wa wateja kuomba kuunganishiwa huduma ya umeme na changamoto zinazosababisha kukatika kwa umeme.

Na Suleiman Abeid,  Shinyanga

WAKAZI wa Kata ya Mwakitolyo wilayani Shinyanga wamelishukuru Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani Shinyanga kwa kuwapatia elimu kuhusiana na taratibu za upatikanaji umeme kwa watu wanaotaka kuunganishiwa huduma hiyo.

Wananchi hao wametoa shukurani zao wakati wa mafunzo mafupi ambayo yamefanyika katika Kijiji cha Mwakitolyo namba tano ambapo wamesema kutokana na elimu waliyopatiwa na Meneja wa TANESCO wameweza kuelewa hatua zinazostahili kufuatwa ili mtu kuunganishiwa umeme.

Pia wamesema katika mafunzo hayo wamepata fursa ya kuuliza maswali kuhusiana na suala la kuchelewa kwa baadhi ya vijiji vyao kupelekewa huduma ya umeme hali ambayo imekuwa ikisababisha wailalamikia Serikali pamoja na watendaji wa TANESCO.

Ofisa Mtendaji wa kijiji cha Nyaligongo, Koyo Ibrahimu amesema elimu waliyopatiwa ataifikisha kwa wananchi wake ili waweze kuelewa hatua ambazo Shirika la TANESCO linachukua hivi sasa ili kuweza kufikisha umeme katika vijiji vyao na ngazi ya vitongoji.

Naye mkazi wa kijiji cha Mahembe kata ya Mwakitolyo wilayani Shinyanga Philipo Malashi amelishukuru Shirika la TANESCO kwa kuanzisha utaratibu mpya wa kuomba umeme kwa kutumia njia za kielektroniki maarufu kwa jina la “Nikonekt” ambao unamuwezesha mteja kuomba umeme kwa kutumia simu yake ya kiganjani.

Malashi amesema utaratibu huo ni mzuri na utaondoa ukiritimba uliokuwa siku za nyuma ambapo mteja alilazimika kusafiri hadi makao makuu ya mkoa kwa ajili ya kufanya taratibu za kuomba kupatiwa umeme.

“Binafsi niwapongeze ndugu zetu hawa wa TANESCO kwa kuanzisha utaratibu huu wa kisasa kabisa, kwa kweli utatupunguzia usumbufu wa kusafiri umbali mrefu kwa ajili ya kwenda kuomba kupatiwa umeme, pia utaokoa muda tuliokuwa tukiupoteza katika uzalishaji wa shughuli za kiuchumi,” anaeleza Malashi.

Kwa upande wake Meneja wa Shirika la Umeme mkoani Shinyanga, Grace Ntungi amesema Serikali hivi sasa imelipatia fedha shirika lake kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya upelekaji umeme vijijini na tayari baadhi ya vijiji umeme huo umeanza kupelekwa ngazi ya vitongoji.

Ntungi amesema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2025 kila kijiji hapa nchini kiwe kimepatiwa umeme ambapo pia itaendelea na mchakato wa kupeleka umeme ngazi ya vitongoji na kwa wilaya ya Shinyanga eneo la Mwakitolyo limepewa kipaumbele kwa vile lina wawekezaji wengi katika sekta ya madini.

“Kwa mwaka huu tumepata fedha hivyo lipo eneo hapa Mwakitolyo namba tano sehemu ya makazi, hali umeme, tunategemea kuanzia mwezi Novemba mwaka huu tuanze kazi ya kuwapatia umeme wakazi wa eneo hilo,”

“Na kama nilivyosema Serikali imejiwekea lengo la kuhakikisha kila kijiji hapa nchini ifikapo mwaka 2025 kiwe kimepatiwa umeme wa REA, walianza na vijiji na sasa yapo maeneo wameanza kufanya tathimini ya kupeleka umeme ngazi ya vitongoji, kikubwa wananchi wetu tuwaombe wawe na subira,” ameeleza Ntungi.


Wakazi wa kata ya Mwakitolyo wilayani Shinyanga wakifuatilia mafunzo yanayotolewa na Meneja wa Shirika la TANESCO mkoani Shinyanga kuhusu taratibu za uombaji umeme kwa njia “Nikonekt.”

Wakazi wa kata ya Mwakitolyo wilayani Shinyanga wakifuatilia mafunzo yanayotolewa na Meneja wa Shirika la TANESCO mkoani Shinyanga kuhusu taratibu za uombaji umeme kwa njia “Nikonekt.”

Meneja wa Shirika la TANESCO Mkoani Shinyanga, Mhandisi Grace Ntungi akiendelea kutoa mada kwa wakazi wa kata ya Mwakitolyo wilayani Shinyanga kuhusu utaratibu mpya wa wateja kuomba kuunganishiwa huduma ya umeme na changamoto zinazosababisha kukatika kwa umeme.


Diwani wa kata ya Mwakitolyo wilayani Shinyanga, Masalu Lusana akifuatilia kwa makini kikao cha Meneja TANESCO mkoa wa Shinyanga, kulia kwake ni Kaimu Ofisa Mtendaji wa kata ya
Mwakitolyo



Ofisa mahusiano wa Shirika la TANESCO mkoani Shinyanga Vicky Senge akitoa somo kuhusu usalama wa umeme kwa wakazi wa kata ya Mwakitolyo wilayani Shinyanga.

Wakazi wa kata ya Mwakitolyo wilayani Shinyanga wakifuatilia mafunzo yanayotolewa na Meneja wa Shirika la TANESCO mkoani Shinyanga kuhusu taratibu za uombaji umeme kwa njia “Nikonekt.”


Wakazi wa kata ya Mwakitolyo wilayani Shinyanga wakifuatilia mafunzo yanayotolewa na Meneja wa Shirika la TANESCO mkoani Shinyanga kuhusu taratibu za uombaji umeme kwa njia “Nikonekt.” Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464