BENKI YA CRDB, SANLAM ZATANGAZA UDHAMINI WA ZAIDI YA SH. MILIONI 350 MASHINDANO YA TAIFA YA MPIRA WA KIKAPU “CRDB BANK TAIFA CUP” 2022


Benki ya CRDB na kampuni ya bima ya Sanlam Life Assurance zimetangaza udhamini wa shilingi milioni 350 kwa ligi ya mpira wa kikapu ya taifa 2022 ijulikanayo kama “CRDB Bank Taifa Cup”. Mashindano hayo yaliyopewa kaulimbiu ya “Nizaidi ya Game Ni Maisha” yatafanyika jijini Tanga kuanzia Novemba 4 na kilele chake ni Novemba 12, 2022.

Akizungumza katika hafla ya kutangaza udhamini huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema benki hiyo imeendelea na uamuzi wake wa kudhamini ligi hiyo ya taifa ya mpira wa kikapu kwa mara ya tatu mfululizo ikiwa ni sehemu ya jitihada za benki hiyo kuwawezesha vijana wa Kitanzania kupitia michezo.

Aliongeza kuwa Benki ya CRDB kupitia Sera yake ya Uwekezaji katika Jamii (CSI Policy) imekuwa ikiwekeza katika michezo ya vijana kwa kuamini kuwa inasaidia kuongeza ushiriki wao katika shughuli mbalimbali za maendeleo katika jamii.
Nsekela anasema Benki hiyo kwa kushirikiana na Sanlam wameamua kuongeza udhamini mwaka huu kulinganisha Shilingi milioni 300 mwaka jana kutokana na mafanikio ambayo CRDB Bank Taifa Cup imekuwa ikiyapata katika miaka miwili iliyopita ambapo vijana zaidi ya 3,000 wameweza kufikiwa.

“Kupitia mashindano haya mbali na kuonyesha vipaji vyao, pia wamekuwa wakipata scholarship za masomo, na kupata mafunzo mbalimbali ambayo yanasaidia kuwajengea kujiamini, kujisimamia na kuzifuata ndoto zao,” alisema Nsekela huku akiishukuru kampuni ya Sanlam kwa kuendelea kuunga mkono mashindano hayo.

Akitangaza zawadi zitakazotolewa kwa washindi wa CRDB Bank Taifa Cup 2022, Nsekela alisema mshindi wa kwanza kwa timu za wanawake na wanaume wataondoka na kitita cha Shilingi Milioni 10 kila mmoja na washindi wa pili wataondoka na kitita cha Shilingi Milioni 5.

“Pamoja na zawadi hizi za timu kutakua na zawadi kwa wachezaji bora wa maeneo mbalimbali na makocha. Jumla ya zawadi zote za fedha taslimu zilizotengwa mwaka huu ni Shilingi milioni 32. Lakini hapo baadae tutakwenda kutangaza zawadi nyengine za ufadhili wa masomo kwa wachezaji watakaofanya vizuri na mwaka huu tutaboresha zaidi,” aliongezea.

Mgeni rasmi katika hafla ya uzinduzi wa CRDB Bank Taifa Cup 2022, Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mchezaji wa Mpira wa Kikapu, Esther Matiko aliipongeza Benki ya CRDB kwa kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kusaidia jitihada za serikali kuendeleza michezo nchini.

Matiko alisema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeweka kipaumbele kikubwa katika michezo kwa kutambua fursa za kiuchumi zinazotokana na sekta hiyo. “Niwapongeze pia kwa kuona umuhimu wa kuweka kipaumbele katika timu za wanawake zinazoshiriki CRDB Bank Taifa Cup. Kwa miaka mingi ushiriki wa wanawake katika mchezo huu umekuwa chini ikilinganishwa na wavulana,” alisema Matiko.

Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania(TBF), Michael Kadebe aliishukuru Benki ya CRDB na Sanlam kwa kuendelea na udhamini wa ligi hiyo huku akibainisha kuwa udhamini wa taasisi hizo kubwa hapa nchini umesaidia kuongeza hamasa na mapenzi ya mpira wa kikapu kwa vijana kama ilivyo kwa mpira wa miguu na michezo mingine.

Kadebe alimueleza Mheshimiwa Matiko kuwa mbali na udhamini unaotolewa na Benki ya CRDB, benki hiyo imekuwa ikishiriki katika kila hatua kuhakikisha mashindano hayo yanafikiwa ikiwamo na kusaidia kushawi taasisi nyimm jngine kushiriki kufanikisha mashindano hayo.

Hafla ya kutangaza udhamini kwa mwaka 2022 ilienda sambamba na mtanange mkali wa timu za wachezaji bora kwa mwaka 2020 na 2021 kwa upande wa wanawake na wanaume. Aidha katika hafla hiyo pia kulichezeshwa droo ya makundi ambapo timu 20 za wanaume na 16 zitachuana vikali.

Mashindano ya CRDB Bank Taifa Cup mwaka 2021 yalifanyika mkoa wa Dodoma katika viwanja vya Chinangali na uwanja wa Jamhuri ambapo vijana 1,000 kutoka kutoka mikoa yote Tanzania bara na visiwani walishiriki. Katika mashindano hayo timu za mpira wa kikapu za mkoa wa Dar es Salaam ziliibuka washindi katika michuano hiyo kwa upande wa wanawake na wanaume.

Mgeni rasmi katika hafla ya uzinduzi wa CRDB Bank Taifa Cup 2022, Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mchezaji wa Mpira wa Kikapu, Esther Matiko akiongoza uchezeshaji wa droo ya Mashindano ya CRDB Bank Taifa Cup 2022 wakati wa ufunguzi rasmi wa msimu wake wa tatu, ulioenda sambamba na mchezo maalumu uliowakutanisha wachezaji waliokuwa bora katika 'CRDB Bank Taifa Cup 2020 na 2021' (MVPs) uliochezwa jana kwenye viwanja vya Don Bosco Oysterbay, jijini Dar es salaam.Picha Zote na Othman Michuzi.

Mkurugenzi wa Bodi ya Benki ya CRDB, Martin Warioba akishiriki uchezeshaji wa droo ya Mashindano ya CRDB Bank Taifa Cup 2022 wakati wa ufunguzi rasmi wa msimu wake wa tatu, ulioenda sambamba na mchezo maalumu uliowakutanisha wachezaji waliokuwa bora katika 'CRDB Bank Taifa Cup 2020 na 2021' (MVPs) uliochezwa jana kwenye viwanja vya Don Bosco Oysterbay, jijini Dar es salaam.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Tully Esther Mwambapa akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa msimu wa tatu wa 'CRDB Bank Taifa Cup 2022, ulioenda sambamba na mchezo maalumu uliowakutanisha wachezaji waliokuwa bora katika 'CRDB Bank Taifa Cup 2020 na 2021' (MVPs) uliochezwa jana kwenye viwanja vya Don Bosco Oysterbay, jijini Dar es salaam.
Meneja wa kampuni ya bima ya Sanlam Life Assurance, Killian Nango akishiriki uchezeshaji wa droo ya Mashindano ya CRDB Bank Taifa Cup 2022 wakati wa ufunguzi rasmi wa msimu wake wa tatu, ulioenda sambamba na mchezo maalumu uliowakutanisha wachezaji waliokuwa bora katika 'CRDB Bank Taifa Cup 2020 na 2021' (MVPs) uliochezwa jana kwenye viwanja vya Don Bosco Oysterbay, jijini Dar es salaam.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464