WATU WAWILI WAUAWA SHINYANGA AKIWAMO MWANAMKE KUCHARANGWA MAPANGA


Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Janeth Magomi akizungumzia matukio ya mauaji hayo mawili.
Wananchi wa kijiji cha Mwamalulu Kata ya Didia wilayani Shinyanga wakiwa kwenye mazishi ya Mwanamke Nshoma Moshi, aliyeuawa kwa mapanga.
Wananchi wa kijiji cha Mwamalulu Kata ya Didia wilayani Shinyanga wakiwa kwenye mazishi ya Mwanamke Nshoma Moshi, aliyeuawa kwa mapanga.

Na Mwandishi wetu, SHINYANGA.

Mwanamke aliyefahamika kwa jina la Nshoma Moshi(50) mkazi wa Kijiji cha Mwamalulu Kata ya Didia halmashauri ya Shinyanga ameuawa na watu wasiojulikana kwa kukatwa mapanga wakati akimuogesha mjukuu wake majira ya saa mbili usiku nyumbani kwake.


Kamanda wa Jeshi la polisi Mkoa wa Shinyanga Janeth Magomi amesema tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo katika kijiji cha Malulu Kata ya Didia ambapo chanzo cha mauaji hayo kikidaiwa kuwa ni ugomvi wa mashamba baada ya mwanamke huyo kushinda kesi mahakamani na kukabidhiwa mashamba yake huku aliyekuwa wakidaiana mashamba ametoroka baada ya tukio hilo.

Kufuatia matukio ya watu kujichukulia sheria mkononi,kamanda Magomi amewataka wananchi kufuata sheria badala ya kusababisha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia ambayo yangemalizwa kwa kushirikisha vyombo husika.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwamalulu Senga Shimba amesema matukio ya mauaji kuanza kutokea katika kijiji hicho yamewashitua na ameliomba jeshi la polisi kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini walimuuwa mama huyo kwakumkata mapanga.

Naye mtoto wa marehemu James Joseph, ameeleza kusikitishwa na tukio la mauaji ya mama yake kuuawa kinyama na watu ambao bado hawajafahamika, na kuliomba Jeshi la Polisi lifanye uchunguzi wa kina ili kubaini wauaji na kupata haki juu ya kifo cha mama yake.

Katika tukio jingine kijana mwenye umri wa miaka 30 aliyefahamika kwa jina la Willison Jogoo mkazi wa Kijiji cha Chembeli Kata ya Didia ameuawa na wananchi wenye hasira kali baada ya kuiba kuku kijijini humo ndipo wananchi waliamuwa kujichukulia sheria mkononi.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464