HALMASHAURI YA USHETU IMEELEZA NI ASILIMIA 44.8 WANAOTUMIA NJIA YA UZAZI WA MPANGO


 Baadhi ya wazazi wakiwa kituo cha afya  wakipatiwa elimu.

Na Kareny  Masasy,Ushetu

HALMASHAURI ya Ushetu wilayani Kahama mkoani Shinyanga imeeleza  wazazi wanaotumia njia ya uzazi wa mpango ni  asilimia 44.8 hadi kufikia  mwezi Septemba  mwaka huu.

Malengo yaliyopangwa ni kufikia asilimia 40  na Vituo vya kutolea huduma za afya  vimekuwa vikitoa elimu mbalimbali juu ya njia za utumiaji.

 Mganga mkuu wa halmahsuari hiyo  Dtk Matindo Athumani  amesema  hayo jana wakati akitoa elimu  kwa wazazi  ambapo ameshauri   wanaume nao washiriki kwenda kliniki na wenza wao kupata elimu ya uzazi wa mpango.

Dkt Matindo ameeleza zipo njia nyingi za kutumia, manufaa ya  uzazi  wa mpango mojawapo ni kuzuia mimba zisizo tarajiwa  na kupanga uzazi wenye manufaa  kwa jamii utakao zingatia  pia ulishaji  bora kwa mtoto na kinga.

“Mpango wa uzazi usipuuzwe kwani unapunguza vifo vya mama vitokanavyo na uzazi, na mama  kupata ujauzito mfululizo  ni kuharisha maisha yake na mtoto”amesema  dkt Matindo.

Mratibu wa afya ya uzazi  mkoa wa Shinyanga  Halima Hamis amesema  wenza wote wawili wanapokwenda kliniki  wanapatiwa elimu ya  namna ya kumtunza mtoto na kupanga uzazi .

“Mkoa wa Shinyanga una asilimia 31 ya wazazi wanaotumia  uzazi wa mpango hivyo ni muhimu mjamzito kuhudhulia kliniki na mwenza ili kufikia malengo” amesema Halima.

Dkt Bingwa wa magonjwa ya watoto  kutoka hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga  Mwita Ngutunyi  amesema  wazazi watumie mbinu ya uzazi wa mpango kupangilia watoto ili walionao waendelee kuwa na afya nzuri.

 Dkt Ngutunyi amesema    wazazi wasipotumia uzazi wa mpango hata   mtoto aliyenaye  ukuaji wake unakuwa sio mzuri hivyo alishauri ujauzito upatikane  kwa mpango.

Sera ya afya ya mwaka 2007 inaeleza afya ya uzazi ni huduma inayotolewa kwa wanawake, wanaume na vijana walio katika umri wa kuzaa ni  huduma jumuishi  ikiwemo elimu ya  uzazi wa mpango.

Tamko la sera  ya afya  ni Serikali  kuandaa  miongozo, mikakati na kuratibu shughuli zinazolenga afya ya uzazi ya makundi mbalimbali pamoja na kuhakikisha huduma za uzazi wa mpango zinatekelezwa.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464