MTANDAO WA WHATSAPP WAKWAMA KUFANYA KAZI KWA ZAIDI YA LISAA LIMOJA

Watumiaji wa huduma mtandao wa kijamii wa WhatsApp wamejikuta wakilazimika kutumia njia mbadala ya kuwasiliana baada ya mtandao huo kuonekana kuwa na shida kwa zaidi ya saa 1 (kuanzia saa 4 mpaka saa 5:30) asubuhi.

Mtandao huo maarufu duniani unaomilikiwa na Kampuni ya META kutoka nchini Marekani umekatika mawasiliano leo Jumanne Oktoba 25, 2022 ambapo watumiaji hawawezi kutuma au kupokea ujumbe au kupigiana simu kupitia mtandao huo.

Hali hiyo imeibua mijadala katika mitandao mingine ya kijamii ikiwamo Twitter huku baadhi ya watumiaji wakilalamika kukosa mawasiliano.

Baadhi ya vyombo vya habari vya kimataifa vimeripoti mtandao huo haufanyi kazi katika nchi mbalimbali ingawa havijataja sababu za mtandao huo kutokufanya kazi.

Mpaka muda huu, tayari mtandao huo umereja tena na kuanza kufanya kazi kwa baadhi ya maeneo huku wamiliki wa META wakiwa hawajatoa maelezo yotote kuhusu hali hiyo.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464