Na Shinyanga Press Club Blog
Shirika la YAWE la mjini Shinyanga limeanza kutoa elimu kwa
jamii juu ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto
katika Kata za Halmashauri ya Shinyanga ,ili kuiwezesha jamii kuwa na uelewa na
kuwafichuwa watu wanaofanya vitendo hivyo kutokana na kukiuka haki za binadamu.
Akizungumza na baadhi ya wakazi wa Kata ya Nyida katika
shule ya Msingi Nyida afisa mradi kutoka Shirika la YAWE Deus Lyakisi amesema
wamelenga kutoa elimu ya kupinga ukatili kwenye jamii na shuleni kupitia mradi
wa Keeping school children safe in Shinyanga utakao tekelezwa Kata ya Nyida,
Didia na Puni kwa ufadhili wa mfuko wa wanawake Tanzania (WFT).
Lyakisi amesema lengo ni kuboresha maisha ya watoto shuleni
na kuwa katika mazingira mazuri ikiwa ni pamoja na kupatiwa mbinu bora za
kujiepusha na vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa watoto na kutoa taarifa za
watu wanaofanya vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Amesema wanalenga kuona mimba na ndoa za utotoni zinapungua
au kuisha, watoto kujitambua na kufanya maamuzi sahihi na kuripoti kesi za
ukatili,jamii kutowatelekeza watoto na walimu kuchukuwa jitihada za
kushughulikia kesi za ukatili ili kukomesha matukio hayo.
Nao baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Nyida wamesema matukio ya
ukatili wa kijinsia bado ni changamoto kubwa kutokana na kuendelea kutokea
katika maeneo mbalimbali na kuiomba serikali kwa kushirikiana na wadau wa
kupinga vitendo vya ukatili kuendelea kutoa elimu.
Kwa upande wake Amos Kadilana mkazi mkazi wa Nyida amekiri
baadhi ya wanaume kufanyiwa vitendo vya ukatili na wake zao lakini wamekuwa
wakiona aibu kutoa taarifa kutokana na hofu ya kuchekwa jambo ambalo
linaendelea kuwaumiza wengi na kurudisha nyuma jitihada za kupambana na vitendo
hivyo.