Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (kushoto) akifanya mazungumzo na Mwenyekiti na Afisa Mtendaji Mkuu wa Visa International, Alfred Kelly kuhusu ushirikiano baina ya taasisi hizo katika kuanzisha huduma za malipo ya kidijitali katika sekta ya utalii. Mkutano huo ulifanyika wakati wa Mkutano wa Viongozi wa Marekani na Afrika Washington DC Marekani siku ya Ijumaa tarehe 16 Desemba 2022.
Washington DC 16 Desemba 2022 - Benki ya CRDB Plc, Benki inayoongoza kwa uvumbuzi
wa kidijitali nchini, na kampuni ya kimataifa ya mifumo ya malipo ya Visa International, leo
wamekubaliana kuhusu ushirikiano wa kuanzisha huduma ya kadi za kidijitali kwa ajili ya
kuboresha huduma za malipo katika sekta ya utalii nchini.
Kupitia kadi hizo, Benki ya CRDB na Visa wanatarajia kutoa njia rahisi zaidi ya kufanya na
kupokea malipo kwa wateja na makampuni ya sekta ya utalii na usafirishaji kwa usalama na
uharaka kulinganisha na mifumo mingine ya malipo.
Ushirikiano huo mpya na Visa, kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB,
Abdulmajid Nsekela, ni hatua muhimu katika kufikia lengo la Benki hiyo katika kuleta
mapinduzi katika mfumo wa kiikolojia wa malipo ya katika sekta ya utalii na usafiri nchini.
“Sekta ya malipo iko katikati ya mapinduzi na kuna hitaji kubwa la makampuni na mamlaka
za utalii na usafiri kusimamia vyema uzoefu mzima wa malipo,” alisema Nsekela.
Aliendelea kusema kuwa, sekta hiyo inazidi kushamiri na kwamba kuna wimbi kubwa la
watalii nchini kutokana na kazi nzuri inayofanywa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
kupitia kipindi cha Televisheni cha ‘Royal Tour’.
Sekta ya utalii nchini Tanzania inazidi kuimarika baada ya janga la UVIKO-19. Ripoti ya
Benki Kuu (BOT) inaonyesha kuwa mapato ya sekta hiyo yameongezeka maradufu hadi
kufikia dola milioni 2,243.8 mwezi Septemba kutoka dola milioni 1,106. Watalii pia
wameongezeka kwa asilimia 63.5 hadi 1,332,476.
Katika muktadha huo, Nsekela alisema kuwa makampuni katika sekta ya utalii na usafirishaji
yanahitaji ufumbuzi wa hali ya juu na muunganisho katika mifumo ya kisasa ya malipo
ambayo itakidhi mahitaji ya wateja wao ambao wengi wanapendelea huduma za kidijitali
ambazo ni rahisi kutumia.
"Ushirikiano huu mpya na Visa utaisaidia Benki ya CRDB katika kuboresha mifumo yake ya
kidijitali hususan katika huduma za kadi, jambo ambalo litakwenda kuboresha uzoefu wa
huduma za malipo kwa taasisi, makampuni na wateja," alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa Visa, Alfred Kelly Jr alisema mfumo
huo wa malipo kupitia Kadi za Kidijitali utakwenda kusaidia kuongeza ufanisi wa malipo na
kutaimarisha mikakati ya malipo kwa wadau wote walio katika mnyororo wa tahamani wa
sekta ya utalii na usafirishaji nchini Tanzania.
"Tunafurahia kuendeleza ushirikiano wetu na Benki ya CRDB, ushirikiano uliojikita zaidi
katika kutumia utaalamu na ubunifu wa mifumo ya malipo kutoka kwa mashirika yote mawili
ili kusaidia kukua kwa sekta ya utalii na usafirishaji," alisema na kubainisha zaidi kuwa
watafanya kazi kwa pamoja ili kufanikisha ajenda ya ujumuishi wa kifedha nchini.
Benki ya CRDB na Visa pia walikubaliana kuanzisha huduma ya kutuma fedha kuvuka
mipaka ili kurahisisha kuchochea biashara na kuwawezesha Watanzania waishio nje ya nchi
kutuma fedha nyumbani kwa urahisi na usalama.
"Rais Samia amefanya kazi kubwa sana ya kufungua nchi; biashara inapanuka, hivyo
tunatakiwa kuweka miundombinu imara ya malipo ili kusaidia kuichochea. Hii ni pamoja na
kuwawezesha Watanzania walioko ughaibuni kuwekeza nchini," alisema Nsekela.
Mkutano kati ya Benki ya CRDB na Visa ulifanyika pembezoni mwa Mkutano wa Viongozi wa
Marekani na Afrika. Mapema mwezi huu viongozi wa mashirika hayo walikutana Qatar,
ambapo yanashirikiana kuwapatia mashabiki wa Kombe la Dunia FIFA huduma za malipo.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464