KISHAPU YAADHIMISHA MIAKA 61 YA UHURU, WATANZANIA WATAKIWA KULINDA TUNU ZA TAIFA


Katibu Tawala wa Wilaya ya Kishapu Shadrack Kengese


Na Stela Paul - Kishapu
Katibu Tawala wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Shadrack Kengese amesema katika kuadhimisha miaka 61 ya uhuru wa Tanganyika, watanzania wanapaswa kujivunia kwa sababu uhuru ulipatikana kwa njia ya amani.

Amesema hayo leo Disemba 9, 2022 kwenye kilele cha maadhimisho ya Miaka 61 ya uhuru ambayo yamefanyika katika Wilaya ya Kishapu.

Amesema waasisi wa taifa hili walipigania uhuru kwa njia ya amani ambayo imeleta misingi bora ya umoja na mshikamano na kwamba misingi hiyo itaendelea kulindwa kwa kuwa ni miongoni mwa tunu muhimu za taifa la Tanzania.

"Katika kuadhimisha miaka 61 ya Uhuru wa Tanganyika, Watanzania wanapaswa kujivunia sana namna ambavyo viongozi wetu walipigania uhuru lakini vilevile waliweka misingi bora ya umoja na mshikamano ambayo inaendelezwa mpaka sasa na viongozi wetu", amesema Kengese.

Kengese amesema katika kuadhimisha miaka 61 ya uhuru, Wilaya ya kishapu imepiga hatua mbalimbali za kimaendeleo katika sekta ya elimu, maji, afya pamoja miundombinu ya barabara hali ambayo imerahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii kwa wananchi.

"Serikali baada ya kupata uhuru iliendelea kuboresha miundombinu mbalimbali ambapo katika wilaya ya Kishapu tumefanikiwa kuboresha miundombinu ya elimu, umeme, afya, maji pamoja na barabara hivyo wananchi mnatakiwa kuilinda na kuitunza miundombinu hii", amesema Kengese.

Baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Kishapu walioshiriki maadhimisho hayo wameipongeza serikali kwa juhudi za kimaendeleo wanazozifanya tangu kupatikana kwa uhuru mnamo Mwaka 1961 na kwamba wameiomba serikali kuendelea kuboresha miundombinu ya barabara katika wilaya hiyo hususani barabara kuu ya Kishapu.

Leo Disemba 9, 2022 Watanzania wameadhimisha kumbukumbu ya miaka 61 ya uhuru wa Tanganyika, ambapo Wilaya ya Kishapu imeadhimisha kwa namna mbalimbali ikiwemo kufanya midahalo pamoja na michezo.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464