Baraza
la Mitihani la Tanzania (NECTA) leo Desemba 1, 2022 limetangaza matokeo
ya darasa la saba kwa mwaka 2022 ambapo limetangaza kufuta matokeo yote
ya Watahiniwa 2194 sawa na asilimia 0.16 ya Watahiniwa 1,350,881
waliofanya mtihani ambao wamebainika kufanya udanganyifu katika mtihani
huo wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2022.
Akitangaza
matokeo ya mtihani wa kumaliza darasa la saba mwaka 2022, Kaimu Katibu
Mtendaji wa Necta, Athuman Amasi amesema pia NECTA imezifungia shule 24
kuwa vituo vya mitihani ya Taifa baada ya kuthibitika kupanga kufanya
udanganyifu katika mitihani ya kumaliza elimu ya msingi.
Shule
hizo ambazo ni sawa na asilimia 0.13 ya vituo vyote vya mitihani
nchini, ndani yake zipo shule maarufu ikiwemo ya Musabe ya jijini Mwanza
na St Anne Marie ya jijini Dar es Salaam na shule ya Rweikiza ya mkoani
Kagera.
Shule
hizo ni Kadama shule ya msingi iliyopo Chato- Geita, Rweikiza (Bukoba),
Kilimanjaro shule ya msingi (Arusha) Sahare (Tanga), Ukerewe (Mwanza),
Peaceland (Mwanza), Karume (Kagera), Al-hikma (Dar es Salaam), Kazoba
(Kagera), Mugini (Mwanza), Busara (Mwanza), Jamia (kagera), Winners
(Mwanza), Musabe (Mwanza), Elisabene (Songwe), High Challenge (Arusha),
Tumaini (Mwanza), Olele (Mwanza), Mustlead (Pwani).
Pia zipo shule za Moregas (Mara), Leaders (Mara), Kivulini (Mwanza) na St Severine (Kagera).
Mtihani huo wa kumaliza elimu ya msingi ulihusisha watahiniwa zaidi ya 1.38 milioni nchi nzima.