Suzy Luhende, Shinyanga Blog
Keflyine Masunga mkazi wa kijiji cha Mwang'hosha kata ya Iselamagazi halmashauri ya wilaya ya Shinyanga aliyeolewa akiwa na umri wa miaka 16 anasimlia jinsi alivyoingia kwenye mtego wa kuolewa wakati akiwa na umri mdogo.
Anasema alianza masomo yake ya darasa la kwanza na kuhitimu darasa la saba baada ya kuhitimu darasa la saba hakufaulu kuendelea na masomo, lakini alimuomba mama yake ampeleke chuo cha Veta ama akajifunze ushonaji, lakini mama yake alikataaa na kumwambia kuwa hawezi kumpeleka kwani akienda huko ataenda kujifunza umalaya.
Keflyine anaeleza kuwa baada ya mama yake kukataa kumpeleka Veta alikaa nyumbani na kuanza kumsaidia mama yake kazi za kuuza mgahawa ambapo alikutana na kijana mmoja akamdanganya kumuowa, aliolewa baada ya muda kidogo wazazi wake walifuata mahali, lakini hawakufanikiwa kupewa mahali ilibidi wanichukue niondoke ili kusudi waje watoe mahali.
"Sisi wasukuma huwa tunapulwa yaani tunachukuliwa bila kuaga nyumba ama bila kufanyiwa sherehe ama harusi baada ya siku mbili kule ulikoolewa wanapeleka taarifa nyumbani kuwa furani yupo kwa furani ameolewa,hivyo wazazi wa upande wa mwanamke wanakwenda alikoolewa mtoto wake kwa ajili ya kudai fedha ya kuibiwa kwa mtoto wao yaani (ya kupulilwa wanaita Ngwekwe) baadae wanarudi kudai mahali sasa.
Anasema fedha hiyo ya ngwekwe walichukua lakini walipoendea ya mahali hawakupewa ndipo wazazi walichukua jukumu la kumrudisha nyumbani akiwa na ujauzito anasema alikaa nyumbani mpaka alijifungua bila kumuona mwanaume hata kuja kulea mtoto na mpaka sasa mtoto ana umri wa mwaka na nusu mwanaume wala hamkumbuki mtoto wake.
"Toka niondoke kwa mme wangu hajaniijia na mtoto hata hamtumii matumizi hata akiugua nahangaika mimi na mama yangu kumpeleka hospitali, halafu aje anidanganye mtu kuniowa siolewi tena nataka kwenda shule ama kujifunza cherehani"anaeleza Keflyine.
Aidha anasema kutokana na shida ambazo amezipata hataki tena kuolewa anataka kusoma ama kwenda chuo cha Veta kujifunza cherehani ili awe na ujuzi na kuweza kujihudumia mwenyewe na kuhudumia mtoto wake.
"Yaani mwandishi unaponiona hivi nahangaika na mtoto wangu hata akija baba yake na mtoto sihitaji tena kuolewa nitafanya juu chini nipate sehemu ya kujifunza cherehani ama nikipata mfadhili wa kunipeleka Veta ama shule yoyote nitaenda niliwahi kuolewa kwa sababu wakati huo nilikuwa sijitambui,"anasimulia Keflyine.
"Nawaomba wadau mbalimbali wanaosaidia wanisaidie ili na mimi niweze kusoma nipo tayari kumuacha na bibi yake mtoto wangu kwa sababu anatembea na anakula mwenyewe napenda sana kusoma baada ya kutofaulu nilimwambia mama yangu nirudie shule alikataa ndio maana yalitokea haya,"anaeleza.
Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Ng'wanhosha John Samson na Shija Hamis wanasema katika mazingira ya vijijini wazazi wengi wanategemea watoto wa kike wabadilishe mazingira ya nyumbani kama mzazi alikuwa hana mifugo anapopata mtoto wa kike anaamini ataolewa na kuleta mahali ya Ng'ombe nyumbani, hivyo ndivyo kubadilika kwa mazingira.
"Ndiyo maana sasa wazazi wengi bado wanaamini kwamba mtoto wa kike ndiyo mtaji mkubwa kwa mzazi kuliko mtoto wa kiume, ndiyo maana baadhi ya wazazi wenye imani hiyo wamekuwa wakiruhusu mtoto kusoma na kuishia darasa la saba na kumshawishi asifanye vizuri mtihani wa kumaliza ili asifaulu aweze kuolewa"amesema Samson.
"Kama anavyoeleza binti yangu huyu kwamba yeye alipenda kuendelea na masomo ijapokuwa amefeli lakini mama yake hakutaka aliona akiendelea na masomo hatapata tena mahali ya Ng"ombe lakini na mategemeo yake yaligonga mwamba aliolewa bila kupewa chochote na kuachiwa mjukuu kulea" anaongeza.
Mbuke Nyanda mkazi wa kijiji cha Ng"waghosha anasema wazazi wasiokuwa na ueleza katika jamii yetu bado wapo lakini wamepungua baada ya kuona viongozi wanawake wameongezeka katika jamii,ukiangalia hata Rais wa Tanzania Samia Suluhu ni mwanamke, hivyo wengi wameanza kubadilika.
"Tunaomba elimu iendelee kutolewa tu ili wazazi wenye kutegemea mahali kuliko kutegemea matokeo makubwa kwa mtoto waweze kuelimika na waweze kusomesha watoto wa kike kwa sababu wanaweza na sasa wanaongoza hata madarasani wanachukua namba nzuri kwenye mitihani yao"anasema Mary Kasanga.
Diwani vitimaalumu wa halmashauri ya Shinyanga Chausiku Salum anasema baadhi ya wananchi wameanza kuwa na uelewa kutokana na kuwepo kwa mashirika mbalimbali ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto, lakini elimu iendelee kutolewa ili wazazi waendelee kuelewa zaidi,
"Tunayashukuru mashirika haya kwa kushirikiana na serikali yanaendelea kuwaelimisha wanawake na wanawake wanaoelimika wanaenda kuelimisha jamii,na tangu elimu oanze kutolewa kuna mabadiliko wengi wameacha kulazimisha kuolewa watoto wa kike, wamebaki wachache nao wataelewa tu,"anasema Chausiku.
Afisa maendeleo wa kata ya Iselamagazi Joyce Chawala anasema kuna baadhi ya wanawake wameeleweshwa na wakaelewa kwamba mtoto wa kike ukimsomesha atarudi kukusaidia tofauti na kukimbilia mahali kwa haraka haraka hata umri wa kuolewa hajafikisha na hata kujitambua mtoto hajajitambua.
"Tunamuona huyu binti Keflyine aliolewa akiwa na miaka 16 lakini mwanaume baada ya kutimiza tu haja zake na kumpa ujauzito hakutaka tena hata kumtolea mahali sasa hivi yupo nyumbani hatumiwi hata fedha ya mayumizi anahangaika na mama yake lakini pia mama bado hajaelewa mtoto amezaa lakini bado anamkataza kujiendeleza hata Veta kwa sababu bado mawazo ya mahali yanamsumbua"anasema Chawala.