Mwenyekiti wa Asasi ya Wanawake Laki Moja Anascholastica Ndagiwe, akitoa tamko kulaani kukithiri matukio ya mauaji ya Wanawake Shinyanga.
Mwenyekiti wa Asasi ya Wanawake Laki Moja Anascholastica Ndagiwe (katikati) akitoa tamko kulaani kukithiri matukio ya mauaji ya Wanawake Shinyanga, (kulia)ni Mwenyekiti wa kikundi kazi cha Mashirika yanayotekeleza afua za kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto (EVAWC Working Group) Paschalia Mbugani, (kushoto) ni Mkurugenzi wa Shirika la Fikra Mpya Leah Josiah.
Utoaji wa Tamko la kulaani kuendelea kwa mauaji dhidi ya wanawake likiendelea.
Na Marco Maduhu, SHINYANGA
ASASI ya Wanawake Laki Moja ambayo inajihusisha na utetezi wa haki za wanawake na watoto mkoani Shinyanga, wamelaani kuendelea kukithiri kwa matukio ya mauaji dhidi ya wanawake mkoani humo.
Mwenyekiti wa Asasi hiyo Anascholastika Ndagiwe, amebainisha hayo leo Januari 16, 2023 wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani Shinyanga, wakati wakitoa tamko la kulaani kuendelea kwa mauaji dhidi ya wanawake Shinyanga.
Amesema Mkoa wa Shinyanga umekithiri kuendelea kwa matukio ya mauaji ya dhidi ya wanawake, na mengi yanatokana na uzembe sababu wanawake hao kabla ya kuuwa wakati na wakitembezewa vipigo na waume zao, wamekuwa wakiomba msaada lakini hawapati hadi wanafikia hatua ya kuuawa.
“Asasi ya wanawake laki moja mkoani Shinyanga tunatoa tamko la kulaani kuendelea kwa mauaji dhidi ya wanawake yatokanayo na uzembe, sababu mtu anaomba msaada lakini hapati akishapoteza maisha ndipo utasikia majirani wakisema alikuwa akiomba msaada, tunaomba tabia hii ife, mtu akiomba msaada asaidiwe ili kudhibiti mauaji, mbona mtu akipiga kelele kuomba msaada wa mwizi watu wanatoka,”amesema Ndagiwe.
Aidha, amesema elimu ya utatuzi wa migogoro inapaswa kuendelea kutolewa kwa wanandoa, sababu ndoa nyingi zilishakufa lakini watu wanaishi tu, na kuwataka wanawake wapaze sauti pale wanapokuwa wakifanyiwa ukatili au kusikia jirani yake akitendewa sivyo, na siyo kukaa kimya mwisho wa siku anapigwa hadi anapoteza maisha.
Naye Mwenyekiti wa kikundi kazi cha mashirika yanayotekeleza afua za kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto mkoani Shinyanga, (EVAWC Working Group) Paschalia Mbugani, amesema mauaji ya wanawake kuendelea kutoka mkoani humo ni uvinjifu wa haki za binadamu.
Ametoa wito kwa wanandoa wanapokuwa na migogoro wasikae kimya, bali wapaze sauti ili wapate msaada wa kusuluhishwa, na kama ikishindikana waachane na siyo kung'ang'ania, sababu ndoa nzuri ni ile yenye Amani.
“Mwanaume akikutamkia kuwa atakuuwa siyo bahati mbaya ipo siku atatekeleza alilodhamiria anakupiga na kukuuwa kweli, hivyo nawasihi wanawake msikae kimya pazeni sauti za matukio ya ukatili,”amesema Mbugani.
Amewaomba pia viongozi wa dini waendelee kutoa mafundisho ya ndoa kila mara na siyo kuishia siku za kufungisha ndoa tu, sababu ndoa nyingi kwa sasa zina migogoro na zinahitaji maombi na mafundisho.
Aidha, Januari 14 mwaka huu katika Kata ya Ngokolo Manispaa ya Shinyanga kumetokea tukio la mauaji ya Mwanamke Joyce Masanja, ambaye ameelezwa aliuawa na Mumewake, na kabla ya mauaji alikuwa akiomba msaada lakini hakupata hadi akapoteza maisha.