MAKAMU WA RAIS DK MPANGO KUWEKA JIWE LA MSINGI HOSPITALI MPYA YA RUFAA SHINYANGA, RELI YA KISASA NA MRADI WA MAJI YA ZIWA VICTORIA TINDE-SHELUI

Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango kuweka jiwe la Msingi Hospitali mpya ya Rufaa Shinyanga, Reli ya kisasa na Mradi wa Maji Ziwa Vitoria Tinde-Shelui.

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Philip Mpango anatarajiwa kufanya ziara Mkoani Shinyanga, ambapo ataweka jiwe la msingi katika Hospitali ya Mpya ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, ujenzi wa Reli ya kisasa na Mradi wa Maji Tinde- Shelui.

Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango atawasili leo mkoani Shinyanga, ambapo kesho ataanza ziara ya kikazi kwa kuweka jiwe la msingi, katika ujenzi wa Reli ya kisasa (SGR) na kisha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, na kesho kutwa januari 19 ataweka jiwe la Msingi katika Mradi wa Maji ya Ziwa Victoria kutoka Tinde kwenda Shelui.

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk. Yahaya Nawanda, ametoa taarifa hiyo leo Januari 17, 2023 wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Hospitali mpya ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.

Nawanda ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, amewataka wananchi wa Mkoa huo wa Shinyanga, wajitokeze kwa wingi kwenye ziara hiyo ya Makamu wa Rais ili kushuhudia uwekaji wa jiwe la msingi kwenye miradi hiyo.

Aidha, akizungumzia ujenzi wa Hispitali hiyo mpya ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kiasi cha Sh,bilioni 9.5 na kufanikisha ujenzi wa hospitali hiyo ambayo tayari imeanza kutoa huduma za matibabu, na imewaondolea adha wananchi wa Shinyanga kufuata huduma za matibabu katika Hospitali ya Bugando na Muhimbili.

“Tunampongeza Rais Samia Suluhu Hassan ametufanyia mambo makubwa hapa mkoani Shinyanga, miradi mingi imejengwa ikiwamo na hospitali hii ya Rufaa ya Mkoa, ambayo itahudumia wananchi wapatao Milioni 2.2 na hakuna tena kwenda Mwanza Bugando wala Muhimbili Dar es salaam sababu huduma zote zipo hapa Shinyanga,”amesema Nawanda.

Amesema Rais Samia ametoa tena fedha katika Hospitali hiyo na kununuliwa vifaa tiba ikiwamo CT-SCAN na Digital X-Ray ambavyo vitaboresha huduma za matibabu kwa wananchi.

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk. Yahaya Nawanda ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu akitoa taarifa kwa waandishi wa habari juu ya ujioa wa ziara ya Makamu wa Rais mkoani Shinyanga Dk. Philip Mpango.

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk. Yahaya Nawanda ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu akitoa taarifa kwa waandishi wa habari juu ya ujioa wa ziara ya Makamu wa Rais mkoani Shinyanga Dk. Philip Mpango.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464