WAKANDARASI UMEME WA REA SHINYANGA WAKALIA KITI CHA MOTO, KUSITISHIWA MIKATABA, MKUDE AGEUKA MBOGO

Muonekano wa nyumba ambayo imefungiwa umeme wa REA kijjini

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

SERIKALI mkoani Shinyanga imeonyesha kutoridhishwa na kasi ya Wakandarasi ambao wanatekeleza mradi wa umeme vijijini REA Mkoani humo, kuwa wanafanya kazi zao kwa kusuasua na tangu wasaini Mikataba Februari Mwaka jana hadi sasa hakuna hata kijiji kimoja ambacho kimewashwa umeme.

Wakandarasi hao walisaini Mikataba mwaka jana 2022, kutekeleza Miradi ya umeme vijijini (REA) katika Wilaya ya Kahama, Shinyanga na Kishapu na Mikataba hiyo itaisha Mwezi Julai mwaka huu, lakini hadi sasa imebainishwa utendaji wao kazi upo chini ya kiwango.

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Joseph Mkude, amebainisha hayo leo Januari 30, 2023 wakati wa kikao cha Tathimini cha Miradi ya meme wa REA mkoani Shinyanga, na Wakandarasi ambao wanatekeleza Miradi ya REA wakiwamo na wawakilishi wa wabunge wa mkoa huo.

Mkude ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Kishapu, amesema katika Mkoa wa Shinyanga Wakandarasi ambao wanatekeleza mIradi ya umeme vijijini REA wanasuasua hawaendi na kasi, huku muda wa mkataba ukikaribia kuisha lakini hawajawasha umeme hata kijiji kimoja.

“Wakandarasi ambao mnatekeleza mradi wa umeme vijijini REA katika Mkoa huu wa Shinyanga, kasi yenu hairidhishi mnatekeleza chini ya kiwango, na Serikali haitasita kusitisha Mikataba yenu,”amesema Mkude.

“Tumeitana hapa leo kufanya tathimini juu ya utekelezaji wa mradi wa umeme wa REA na kutiliana mkazo utekelezwe ndani ya muda wa Mkataba, na Mpaka sasa hamjawasha umeme hata kijiji kimoja na Mkataba unaisha Julai mwaka huu, na mnabahati Waziri wa Nishati Januari Makamba amewapa mwezi mmoja na nusu aone utekelezaji wake, ingekuwa sisi ni wiki mbili tu,”ameongeza

Aidha, amewataka Wakandarasi hao wanapokuwa wakitekeleza miradi yao ya umeme vijijini, kila baada ya wiki moja watoe taarifa kwenye Ofisi ya Mkuu wa wilaya ili kufuatilia maendeleo yao na kuona kasi inakwendaje.

Naye Mkurugenzi wa Uendelezaji Masoko na Teknolojia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Advera Mwijage, amesema katika Mkoa huo wa Shinyanga Wakandarasi wanatekeleza mradi wa REA chini ya kiwango, na tangu wasaini Mikataba yao mwaka jana mwezi Februari hakuna hata kijiji kimoja kimewashwa umeme hadi sasa, na Mkataba utaisha Julai mwaka huu.

Amemtaja Mkandarasi kutoka Kampuni ya Tontan Project Technology Co.LTD ambaye anatekeleza mradi wa umeme wa REA wilayani Kahama, kuwa ana vijiji 146 na katika utekelezaji wake yupo asilimia 25 na kwamba alipaswa hadi sasa awe amefikia asilimia 44 hivyo kasi yake hairidhishi.

Amemtaja pia Mkandarasi mwingine kutoka SUMA JKT ambaye anatekeleza mradi wa umeme wa REA wilayani Shinyanga na Kishapu, kuwa ana vijiji 101 na mpaka sasa alipaswa awe amefikisha asilimia 55 ya utekelezaji, lakini yupo asilimia 28 na yeye hakuna hata kijiji kimoja ambacho amewasha umeme.

Amesema Wakandarasi hao walipatikana kwa njia ya ushindani na nyaraka zao zipo vizuri na kuonyesha uwezo wa kitaalamu pamoja na kifedha kutekeleza miradi, lakini wanasikitika kuona uwezo wao unakuwa mdogo na kufanya kazi chini ya kiwango, na kusema hawata ongeza muda wa utekelezaji.

Alisema pia watafuata utaratibu wa kuripoti Wakandarasi ambao wanawasumbua na kushidwa kutekeleza miradi kwa wakati kwa bodi ya usajili ya Wakandarasi na Mamlaka zingine ikiwamo PPRA, na Wakandarasi ambao siyo wa nchi hii watawaripoti kwenye balozi zao.

Naye Msimamizi wa mradi wa umeme wa REA kutoka SUMA JKT Meja James Mhame, ambao wanatekeleza mradi huo wilayani Shinyanga na Kishapu, amesema tatizo ambalo limekwamisha kushindwa kutekeleza mradi huo kwa kasi nikutokana na mvua kunyesha na kusababisha magari kushindwa kupita, huku akiahidi kuongeza kasi na hadi kufikia Julai vijiji vyote 101 vitakuwa na umeme.

Msimamizi wa Kampuni ya Tontan Project Technology Co.LTD ambao wanatekeleza mradi wa umeme wa REA wilayani Kahama Mhandisi Revocatus Silvester, ameahidi kutekeleza maagizo hayo na kusema kuwa ndani ya wiki moja watakuwa wameshawasha umeme katika vijiji 10, na hadi kufikia mwisho wa Mkataba Julai mwaka huu vijiji vyote 146 vitakuwa na umeme.

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Joseph Mkunde akizungumza kwenye kikao cha Tathimini juu ya kusuasua kwa utekelezaji wa mradi wa Umeme wa REA Mkoani Shinyanga.

Mkurugenzi wa Uendelezaji Masoko na Teknolojia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Advera Mwijage akizungumza kwenye kikao hicho.

Kikao cha Tathimini utekelezaji mradi wa Umeme wa REA mkoani Shinyanga kikiendelea.

Wajumbe wakiendelea na kikao.

Wajumbe wakiendelea na kikao.

Wajumbe wakiendelea na kikao.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464