KUSHINDA NJAA KWA WANAFUNZI KUNASABABISHA WANAFUNZI KUTOFAULU VIZURI MASOMO YAO


Suzy Luhende, Shinyanga  Blog

Wazazi na walezi katika kata ya Iselamagazi halmashauri ya Shinyanga wamekuwa ni chanzo cha watoto wao kutofaulu  vizuri masomo kutokana na wazazi hao kukataa kuchangia chakula mashuleni, hivyo kuwafanya watoto hao kushinda njaa kuanzia asubuhi hadi jioni saa 12 hadi saa moja usiku hivyo kula mara moja kwa siku.

Akizungumza na Shinyanga Blog mwalimu mkuu wa shule ya sekondari Iselamagazi Sositenes Chisaki amesema ili wanafunzi waweze kufundishwa na kuelewa masomo  wanatakiwa wawe wameshiba lakini wanafunzi wa shule hiyo wamekuwa wakishinda njaa kutokana na wazazi wao kukataa kuchangia chakula.

"Mwanafunzi ili aelewe vizuri anachofundishwa anatakiwa awe amekula ameshiba, lakini watoto hawa tunawafundisha kuanzia asubuhi mpaka jioni wakiwa na njaa kutokana na wazazi wao kukataa kuchangia chakula,"amesema Chisaki.

"Baada ya kuona baadhi ya wanafunzi  wanasinzia darasani tukachunguza na kugundua kuwa wanakuwa na njaa, tuliwaita wazazi na kuwaomba wachangie chakula ili wanafunzi hao wawe wanapikiwa chakula shuleni hapa lakini wazazi walikataa kabisa na kusema wao hawachangii hawana chakula wala fedha,"ameongeza Chisaki.

Baadhi ya wazazi Mayunga Nkwabi na Jesca Dotto wamesema wazazi wengi hawakutaka kuchangia kutokana na hali ya chakula kuwa mbaya, wengi walikuwa hawana chakula majumbani kutokana na mvua kuwa chache, hivyo hawakuivisha vizuri mazao ya chakula.

"Labda mwakani tunaweza kuchangia tukiivisha mazao yetu tunayotarajia kulima, lakini kwa sasa hatuna chakula tunanunua unga kwa kilo, mchele kwa kilo, hivyo hali ni mbaya sana watusamehe tu kwa mwaka huu jamani watakuwa wanakuja kula nyumbani wakirudi jioni,"amesema Dotto.

Nao baadhi ya wanafunzi wa shule ya Iselamagazi George Erick na Ester wamesema wazazi wao  wamekuwa ni wagumu sana kuchangia chakula, hivyo wameshazoea wanakula usiku na kula usiku mwingine, hali ambayo inawafanya hata vipindi vyote wasivisikilize ipasavyo kwa sababu ya njaa.

Kwa upande wake afisa maendeleo wa kata ya Iselamagazi Joyce Chawala amesema kweli wazazi ni wagumu sana kuchangia chakula kwani tayari wameshaitwa shuleni na kushirikishwa kwa ajili ya kuchangia, lakini walikataa na wengine alijaribu kuwashawishi ili kuweza kuwasaidia wanafunzi angalau waweze kuchangia lakini mpaka leo kimya.

" Na hali hii inaweza kusababisha watoto wa kike kushawishika kwa boda boda, wakidanganyiwa chipis tu,tunawaomba wazazi wabadilike ili  wachangie chakula kwa ajili ya watoto kwani wengi wanasema hawana chakula na hawana fedha za kuchangia, lakini hii inawaumiza sana watoto hawa inawafanya wasisikilize ipasavyo vipindi vya masomo kwa sababu ya njaa lakini wanatakiwa wabadilike wawe na huruma kwa watoto wao kwa sababu ni Tegemeo lao la kesho,"amesema Chawala.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464