Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi wilaya ya Shinyanga Shija Ntelezu akizungumza kwenye kikao cha baraza
la madiwani
Suzy Luhende Shinyanga Blog
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM wilaya ya Kishapu Shija Ntelezu amewashauri madiwani wa halmashauri hiyo na watendaji wake kujiondoa kwenye chama cha ushirika Shinyanga Shirecu badala yake waunde chama chao cha ushirika kutoka Kishapu.
Hayo ameyasema jana wakati akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani cha kujadili na kupitisha mpango wa bajeti wa mwaka 2023/2024 wenye jumla ya Sh 39.4 bilioni ya halmashauri ya wilaya ya Kishapu ambayo itatumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo iliyoainishwa .
Ntelezu alisema Kishapu ikiunda chama chake cha ushirika watakuwa na tani za kutosha na wataweza kukopesheka vizuri kwa sababu wana watendaji wazuri na maafisa ushirika wa kutosha katika halmashauri ya Kishapu.
Kwa upande wake mwenyekiti wa halmashauri ya Kishapu William Jijimya amesema watalamu na madiwani waendelee kufanya maboresho ya kilimo cha pamba kulima kwa kufuata utaratibu wa kilimo cha pamba ili kuweza kujikwamua kiuchumi.
"Tuwahimize wananchi wetu waendelee kulima mazao yanayositahimili ukame na mazao ya biashara kama choroko, arizeti na mtama na tulime kwa wakati kwa kufuata utaratibu na sheria za kilimo na pia nawaomba wazazi mkawasisitize wazazi wawahimize watoto waende shule,"amesema Jijimya.
Katibu tawala wa halmashauri ya Kishapu Shadrack Kengese amesema mwaka huu mvua zinanyesha, hivyo amewataka wakasimamie wananchi walime mazao yanayositahili ukame ili waweze kupata chakula cha kutosha.
Baadhi ya madiwani Edward Manyama wa kata ya Kiloleli na Joel Ndetoson diwani wa kata ya Kishapu wamesema ushauri alioutoa mwenyekiti wa Chama cha mapinduzi CCM ni mzuri kwa sababu Kishapu ikijiondoa kwenye chama cha ushirika itajiongezea mapato na wananchi watajikwamua kiuchumi
Madiwani wa halmashauri ya Kishapu wakiendelea kujadili bajeti ya mwaka 2023/2024
Madiwani viti maalumu wakiendelea kuchakata mpango wa bajeti
Mwenyekiti wa halmashauri ya Kishapu William Jijimya akizungumza kwenye kikao cha bajeti