SHULE SHIKIZI BADO ZINAHITAJIKA KUMKOMBOA MTOTO KUTEMBEA UMBALI MREFU


Mojawapo ya shule shikizi zilizojengwa mwaka jana mkoani Shinyanga.

Kareny Masasy

WAZAZI waelewe shule zilizopo  ni mali yao wanawajibu wa kuanzisha shule shikizi ili kuweza kuwakomboa watoto kutembea umbali mrefu nakuendana na sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014.

Sera hiyo inaeleza uandikishaji wa watoto darasa la awali ni kuanzia umri wa miaka  minne na mitano.

Baadhi ya wazazi wanaoishi pembezoni mwa kata ya Lyabukande halmashauri ya wilaya ya Shinyanga  wanahitaji shule shikizi ili wanafunzi wasitembee umbali mrefu.

Mkazi wa kitogoji  cha Mwazagamzaga kata ya  hiyo Doris Masome anasema   shule za msingi ziko mbali watoto wenye   umri wa miaka minne au mitano hawezi.

Hanowa  Jilinde anasema  watoto wao kuwaanzisha darasa la awali wakiwa na umri wa miaka saba  na nane  tayari wanaweza kumudu kutembea safari ndefu.

“Baadhi ya wazazi bado wana hofu na  watoto wao kupotea njiani wakati wa kurudi na kwenda shuleni”anasema Jilinde .

Solomon  Deus anasema shule ingekuwa karibu hata miaka minne inayoelezwa na serikali kuanza shule ingewezekana kwa watoto.

Mwenyekiti wa kijiji cha Lyabukande  Peter Labacha anasema  shule ipo kwenye eneo la makao makuu ya kata lakini vitongoji havina shule wanalazimika watoto  wenye umri wa miaka sita kutembelea kilomita zaidi ya tano.

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Lyabukande  Jeremiah  Mashaka anasema watoto wengine wameletwa wakiwa na umri wa miaka nane kuanza  darasa la awali.

Mwalimu Mashaka anasema baadhi ya wazazi bado wanawaleta watoto umri mkubwa wakati angetakiwa umri wa miaka minne wanadai  shuleni  iko mbali watoto watapotea.

“Nilikwisha waambia tufanye utaratibu  wa kuanzisha ujenzi wa  shule shikizi ili watoto waweze kupata elimu ”anasema  Mwalimu Mashaka.

 Mwalimu Mashaka anasema nimeandika watoto 60  walioletwa wenye umri wa miaka sita na saba na watoto 26 wenye umri wa miaka zaidi ya 10 kuanza darasa la awali.

Mwalimu anayefundisha darasa la kwanza  Leticia  Obadia anasema watoto wenye umri mkubwa  moja kwa moja huanzishwa darasa la kwanza pale ambapo  wanaonekana kujua kusoma ,kuandika na kuhesabu.

Mwalimu Obadia anasema  asipozijua hurudishwa darasa la awali ili kwenda kuzijua  KKK  akishafahamu vizuri kwa  muda mfupi huendelea na darasa la kwanza.

Mratibu elimu kata hiyo Harun Ibrahim anasema  jiografia ya kata hii imekaa vibaya kwani kuna vijiji saba  na kila kijiji kina shule ya msingi na darasa la awali.

Ibrahim anasema kutoka kitongoji kimoja kwenda kingine ni umbali wa kilomita tano hadi nane  na  miundombinu ya barabara ni mibovu.

“ suala la kuanzisha shule shikizi liliongelewa kwenye mkutano wa hadhara lakini hakuna mtu  ambaye alikuwa tayari  kutoa eneo lake ijengwe shule”anasema  Ibrahimu.

Mtendaji wa kata Shadrack  Malando anasema  anasubiri jamii ivune mazao nakuweka msisitizo wa pamoja lipatikane eneo ili shule ianzishwe.

Ofisa elimu msingi Christina  Bukori anasema  kuna shule za msingi 139  ambazo zina madarasa  ya awali na halmashauri nzima ina shule shikizi mbili tu.

“Shule niza jamii  wa eneo husika hivyo sisi tunawapa maarifa namna ya kuondoa changamoto hizo ni kupambana kwa kuanza ujenzi wa shule shikizi”anasema Bukori.

Ofisa  elimu mkoa  wa Shinyanga   Dafroza Ndalichako anasema mwaka 2022  zilijengwa shule shikizi 60  katika maeneo tofauti tofauti na kuna shule za msingi 644 zenye madarasa ya elimu ya awali.

Ndalichako anasema changamoto iliyopo  baadhi ya wanafunzi  wa madarasa ya awali na kwanza wanatoka maeneo ya mbali  na shule .

Ndalichako anasema  mikakati iliyopo kuweka shule shikizi  karibu na ili watoto wote waweze kupata fursa ya elimu kuanzia darasa la awali.

Mtaalamu mshauri wa malezi na makuzi ya watoto kutoka  Children in Crossfire ( CiC )  Davis Gisuka  anasema umbali wa shule unamkatisha tamaa  mtoto kupenda shule.

“Kwanza  safari inakuwa imemchosha anapofika darasani atataka kulala nakutosikiliza kitu chochote  ambapo atatoka hajui kuhesabu,kuandika hata kusoma mwaka mzima”anasema Gisuka.

Gisuka anasema faida ya mtoto kumuanzisha shule umri mdogo anapata uchangamfu na uelewa wa mapema kuliko mwenye umri mkubwa wakati mwingi akaichukia shule.

Wadau wa elimu  akiwemo mtathini na mfuatiliaji kutoka shirika la Thubutu Africa Initiatives (TAI) Paschalia Mbugani anasema  athari za umbali wa shule kwa watoto unachangia kutomaliza shule na utoro wa rejareja.

Ilani ya  uchaguzi ya chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 -2020  imeongeza  idadi ya shule za msingi zenye madarasa  ya elimu ya awali

Ambapo kulikuwa na  madarasa  16,889 mwaka 2015 hadi kufikia  madarasa 17,771 mwaka 2020.

Sera ya elimu na mafunzo  ya mwaka 2014  ili kujumuisha  elimu  ya awali  katika elimu ya msingi kwa kuzitaka shule zote za msingi kuwa na madarasa ya  elimu ya awali na watoto umri miaka minne na mitano kuandikishwa.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464