UKOSEFU WA ELIMU,UMASIKINI NA TAMAA VYASABABISHA UKATILI WA KIJINSIA


Elipendo John akiwezesha jukwaa la wanawake katika kata ya Iselamagazi 

  Suzy Luhende, Shinyanga Blog 


Imeelezwa kuwa sababu inayosababisha ukatili wa kijinsia katika jamii ni ukosefu wa elimu,umasikini, Tamaa, kuchanganyikiwa na kutokuelewana ndani ya familia na ndani ya jamii yenyewe.

Hayo yameelezwa na wanawake wa kata ya Iselamagazi wakati wakiwa kwenye jukwaa la wanawake lililoundwa na  Yoang Women Lidership (YWL)  kwa ufadhili wa Women Fund Tanzania -Trust  WFT lililofanyika kijiji cha Ichongo halmashauri ya Shinyanga ambalo limeundwa kwa ajili ya kutoa elimu na kutokomeza  ukatili wa kijinsia wilayani hapo.

Wakiwa katika majadiliano wanawake hao wamesema changamoto kubwa inayosababisha ukatili wa kijinsia katika jamii ni ukosefu wa elimu, labda ikitolewa elimu mara kwa mara wananchi wengi watabadilika na watu wakibadilika na kufanya kazi kwa bidii umasikini na ukatili hautakuwepo tena, na wanawake na watoto watakuwa na amani.

Wakitoa hoja mbalimbali katika jukwaa hilo  Zahra Isumari mkazi wa kijiji cha Mwabundala na Suzana John mkazi wa kijiji cha Ibubu wamesema changamoto hizo zikipungua katika jamii amani itatawala na upendo utakuwepo cha muhimu elimu iendelee kutolewa ili  jamii iweze kubadilika.

Wanawake hao wamesema kuna madhara makubwa sana katika kufanya ukatili ukiwemo ulemavu wa kudumu, kifo, magonjwa ya kuambukiza, kusababisha watoto wa mitaani, kushuka kwa uchumi wa familia, kutokupata haki ya elimu, kutokujiamini kisaikolojia.

" Sisi tuliopata mafunzo haya tutaenda tukawape elimu hii hata majirani zetu watoto wetu na ndugu zetu, pia pale tutakapoona kuwa kumefanyika jambo la ukatili hatutasita kutoa taarifa kwa uongozi wa juu ama kwenye mashirika yanayotete na kukemea ukatili," amesema, Suzana John.
Afisa maendeleo wa halmashauri ya Shinyanga Aisha Omary amesema tayari elimu inaendelea kutolewa katika jamii tatizo bado kuna watu wameshikilia mira na desturi lakini wakiachana nazo na kubadilika na kusikiliza elimu inayotolewa changamoto za ukatili zitapungua na wakati mwingine kuisha kabisa.
Afisa mtendaji wa kata ya Iselamagazi Amos Daud amesema baadhi ya wananchi wanabadilika kulingana na elimu inavyoendelea kutolewa lakini kuna wengine elimu imekuwa ikiwafikia wanapuuzia wanaona hayo ni mambo ya wanawake tu wanafundishwa, lakini toka elimu itolewe kuna wanawake wengi na wanaume baadhi wameelewa.

Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Yoang Women Lidership Beatrice John amewataka viongozi wa jukwaa waliopatiwa mafunzo wanatakiwa wakawe mabalozi wa kutoa elimu juu ya ukatili wa kijinsia ili jamii iweze kuelewa na kubadilika.

Baadhi ya wanaume Masalu Nyolobi na Yuduph Ndanya wamesema mara nyingi wanaona mashirika mengi yanafika kijijini hapo kwa ajili ya wanawake tu, ili jamii yote ibadililike hata wanaume wanatakiwa kupewa semina hivyo mashirika yaangalie upya kwamba hata wanaume wanastahili kupewa elimu ya ukatili maana wao ndio waanzilishi wa ukatili.








Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464