Baadhi ya wanaume wa kata ya Iselamagazi halmashauri ya Shinyanga wameshauriwa kuachana na tabia ya kukimbilia madada poa ambao wamekuwa wakivamia nyakati za mavuno katika sehemu za senta za vijiji ambao wamekuwa wakiwasababishia wanaume kubeba magunia ya mpunga na kuwapelekea ili waweze kushiriki nao kimapenzi.
Ushauri huo umetolewa na wanawake wa kata hiyo walipokuwa kwenye jukwaa la wanawake linaloelimisha jamii na kupunguza ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto, ambapo katika majadiliano waliwashauri wanaume kuachana na wanawake wanaoenda kuuza miili yao maarufu kwa jina la (madada poa) ambao wamekuwa wakivamia vijijini nyakati za mavuno na kusababisha vilio na umasikini mkubwa ndani ya familia.
Modesta Simon mkazi wa kijiji cha Ibubu na Suzana John wamesema licha ya kutolewa elimu mara kwa mara, lakini wanaume hawabadiliki, wamekuwa wakibadilika pale wanapoishiwa na kuhakikisha magunia ya mpunga yameisha ndani, ndio wanakuwa wapole na kurudi nyumbani,wakiwa hawana kitu.
"Wakati wa kilimo tunashinda mashambani kwa ajili ya kilimo, lakini tunapoivisha tu madada powa mnawaona wanaanza kutua senta, na baadhi ya waume wanapowaona wanaanza kushindana kwa kuhonga magunia ya mpunga ambao wanaume wamekuwa wakienda kuchukua kwenye familia zao kwa nguvu bila makubaliano na wenza wao na mwanamke akiuliza chochote juu ya mpunga huo anapigwa,"amesema Suzana.
"Wanawake wengi wamekuwa wakiteseka sana wakati wa mavuno ukizingatia wakati wa kilimo wanashinda shambani lakini anapotegemea kupumzika baada ya kuvuna anajeruhiwa kwa kubebewa mazao yake aliyoyahangaikia kwa kutumia nguvu yake, inauma sana tunawashauri tu wanaume mbadilike muache kuwakimbilia hawa madada powa wanaotoka mjini kuja kutuibia mazao yetu,"amesema Modesta.
Mery Reonard mkazi wa kijiji cha Homango amesema baadhi ya wanaume wasio na msimamo ndiyo wamekuwa wakirubunika na kuchukua mali za familia na kwenda kuzihonga kwa wanawake wanaouza miili yao kipindi cha mavuno, hali inayosababisha baadhi yao kutelekeza familia zao wakihamia huko.
“Tunakuwa na furaha wakati wa kilimo lakini wakati wa mavuno tunalia na wanaotuliza ni hawa wanawake wenzetu, wanakuja kwa ajili ya kuuza miili yao,tunaiomba serikali ituhurumie ivikatae kabisa vitendo hivi ambayo vinasababisha mali za familia kupotea lakini pia ni chanzo cha maambukizi ya magonjwa ya zinaa pamoja kupata maambuzi ya Virusi vya Ukimwi VVU”, amesema Mery.
Shija Kisala mkazi wa kijiji cha Mwang"hosha alisema wamekuwa wakiwashauri wanaume kuacha tabia ya kuuza mali za familia na kupeleka kwa wanawake wanaojiuza, kwani kitendo hicho ni sawa na kuibia familia na kuiacha ikihangaika kinachotakiwa wabadilike wanaofanya vitendo hivyo, na wajari familia zao .
Mtendaji wa kata ya Iselamagazi Amos Daudi amesema kesi nyingi za mme na mke zimekuwa zikitokea wakati wa mavuno kina mama wengi wamekuwa wakifika ofisini wakilia kwa madai kuwa wamepigwa na wenza wao wakati wakikatalia mpunga, hivyo wamekuwa wakiwashauri wanaume waache tabia ya kujiibia wenyewe badala yake watunze familia zao.
Kwa upande wake afisa maendeleo wa kata hiyo Joyce Chawala amesema kweli wakati wa mavuno wamekuwa wakivamia wanawake wengi kutoka sehemu mbalimbali na wanakuja kwa madai kuwa wanatafuta kazi za uhudumu wa baa wanapopata wanapanga vyumba na wanaume wanahamia kwenye vyumba vyao na kuanza kusomba pole pole mpunga na kupeleka kwa mwanamke mpya aliyempata.
"Wakati kama huu wa kilimo huwezi kuwaona hao wanawake utawaona wakati wa mavuno na wanaume wengine wanahamia huko huko na kusahau kabisa famili zao, wanawake tumekuwa tukiwashauri wavumilie kwa ajili ya kukuza watoto maana mwanamke nae akiondoka watoto wanapata shida, hivyo wanawake wengi wanavumilia kwa ajili ya kulea watoto wao,"amesema Chawala.