WANAWAKE WAFANYISHWA KAZI WANAPOTOKA KUJIFUNGUA



Suzy Luhende, Shinyanga Blog
Baadhi ya wananchi wa kata ya Iselamagazi katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wameiomba serikali na wadau mbalimbali kuielimisha jamii juu ya ukatili wa kijinsia, kwani wanawake wamekuwa wakifanyiwa ukatili na baadhi ya wanaume wakati wakitoka kujifungua, ambapo hutakiwa kufikia jikoni na kuanza kumpikia mme wake na kumfulia nguo bila kujua kuwa huo ni ukatili.

Hayo wameyasema jana wakati wakizungumza na mwandishi wa habari aliyetembelea katika kata hiyo, ambapo wamesema matukio mbalimbali ya ukatili yanatokea yakiwemo ya akina mama kufanyishwa kazi wanapotoka hospitali baada ya kujifungua na wakati wanapougua, hulazimishwa kupika na kufanya kazi zingine.

Mwenyekiti wa jukwaa la wanawake kijiji cha Ichongo Mary Kasanga amesema baadhi ya wanawake wamekuwa wakifanyishwa kazi na waume zao bila kujua kama wanajiumiza wenyewe, unakuta mwanamke ametoka hospitali kujifungu anapofika nyumbani anapitiliza jikoni kumpikia mme wake na mwingine kupitiliza shambani bila kujua kwamba baadae anaweza kupata madhara, hivyo elimu itolewe ili kuokoa afya za wanawake.

"Tunaomba sana elimu itolewe kuna baadhi ya wanaume hata wanawake hawajui maana ya ukatili ndiyo maana hata hawawasaidii wenza wao hata wakiwa wanatoka hospitali kujifungua hawawasaidii kupika kufua, wanapoumwa lazima waingie jikoni kupika kwa ajili ya waume zao na watoto hivyo tunaomba serikali na wadau mbalimbali walete elimu ili wanaume waache kuwatesa wanawake jamani,"amesema Mary.

Christina Piter mkazi wa kata ya Iselamagazi amesema baadhi ya wanaume wengi hata wanapoona wanawake wameitwa kupewa elimu wanawakataza kwamba wataenda  kufundishwa vibaya waache kuwaheshimu,hivyo ndiyo maana wanawake wengi hawajitokezi hata kwenye vikao mbalimbali vya kimaendeleo.

Afisa maendeleo wa kata ya Iselamagazi Joyce Chawala amesema kweli wanawake wengi wanafanyiwa ukatili ila kwa sababu hawajui nini maana ya ukatili wamekuwa wakifanyiwa na kuona kawaida tu.

Kwa upande wake mratibu wa MTAKUWWA wa halmashauri ya Shinyanga vijijini Aisha Omary amesema Ili kuondokana na hali ya ukatili Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inaendelea kutoa elimu kwa wanawake na makundi yote ambayo yamekuwa yakifanyiwa ukatili, ili yatambue aina zote za ukatili na namna ya kupata msaada.

"Nawaombeni wanawake mpaze sauti msinyamaze kimya pale mnapofanyiwa ukatili ndani ya familia kwa hofu ya kuogopa kuvunja ndoa zenu, mkiendelea kufanya hivyo  kuna madhara makubwa yanaweza tokea  kuliko kutetea ndoa  mnazozilinda, pazeni sauti ili kuokoa ndoa na kuokoa afya zenu na maisha yenu,"amesema.





Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464