WACHINA MRADI RELI YA KISASA ‘SGR’ WAVAMIWA, MLINZI AFUNGWA KAMBA ANYANG’ANYWA SILAHA, MAJAMBAZI 9 WADAKWA


Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Janeth Magomi akionyesha madumu yenye mafuta ya Dizel ambayo yameibiwa katika mradi wa ujenzi wa Reli ya kisasa SGR.

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

WATU Tisa ambao wanasadikiwa kuwa ni Majambazi wamekamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga, ambao walivamia kambi ya wachina iliyopo Oldshinyanga Manispaa ya Shinyanga wanaojenga mradi wa Reli ya kisasa (SGR) na kupora fedha za kigeni.


Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Janeth Magomi, amebainisha hayo leo Februari 6, 2023 wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, kufuatia msako ambao wameufanya ndani ya wiki mbili kuanzia Januari 24 hadi Februari 5 mwaka huu.

Amesema tukio hilo la ujambazi limetokea Februari 4 mwaka huu kwenye Kambi hiyo ya wachina ya wachina Oldshinyanga, na kufanikiwa kuwakamata majambazi Tisa pamoja na fedha za kigeni ambazo ziliibiwa.

“Majambazi hawa wakati akitekeleza tukio la wizi walimfunga pia mlinzi kamba ambaye alikuwa akilinda Kambi hiyo ya wachina, na kuchukua bunduki aina ya Shortgun Pump Action ambayo waliondoka nayo, lakini waliitelekeza tena ,”amesema Magomi.

“Katika tukio hili la ujambazi tulifanikiwa pia kukamata fedha za nchi mbalimbali, Naira 16,000 za Nigeria, Dollar 100,500 za Vietnam, Yuan 20 za Kichina, Dinar 1.5 za Kuwait na Rial 900 za Cambodia na uchunguzi ukikamilika majambazi hawa tutawafikisha mahakamani,” ameongeza.

Katika hatua nyingine Kamanda amesema Jeshi la Polisi limekamata madumu yakiwa na mafuta ndani aina ya Dizeli lita 910 mafuta yalioibiwa katika ujenzi wa Reli ya kisasa (SGR) zikiwamo na Pikipiki Nane zilizotumika katika wizi wa mafuta hayo.

Katika hatua nyingine Kamanda ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga hususani vijana, kuacha tabia ya kuhujumu mradi wa Reli ya kisasa (SGR) na kuiba vitu mbalimbali.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464