RPC MAGOMI ANG’AKA ASKARI KUVUJISHA SIRI TAARIFA ZA UHALIFU, AKAMATA LITA 780 ZA MAFUTA YALIYOIBWA UJENZI MRADI SGR



Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Janeth Magomi akitoa taarifa kwa vyombo vya habari

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

KAMANDA wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Janeth Magomi, amekemea tabia ya baadhi ya Askari wa Jeshi hilo ambao siyo waadilifu, na wamekuwa wakivujisha siri taarifa za uhalifu ambazo wamekuwa wakipewa na wananchi.

Magomi amebainisha hayo leo Februari 27, 2023 wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kufuatia misako na doria aliyoifanya kwa kipindi cha kuanzia Februari 5 hadi 27 mwaka huu.

Amesema Jeshi hilo linakemea vikali tabia ya baadhi ya Askari wachache wasio waadilifu ambao wanavujisha siri juu ya taarifa za uhalifu ambazo zinatolewa na wananchi, hali ambayo inadhoofisha kwa upatikanaji wa taarifa za uhalifu, na kubainisha kuwa watakaobainika kuendelea kufanya hivyo watachukuliwa hatua kali za kinidhamu.

“Jeshi la Polisi linaongozwa kwa miongozo (Polisi General order) kwa hiyo ndani ya Jeshi la Polisi tunachukulia hatua za kinidhamu ikiwamo adhabu mbalimbali na hata kufukuzwa kazi, hivyo Jeshi la Polisi tunatakiwa kufanya kazi kwa weledi, nidhamu na kuhakikisha hatuvujishi siri na kikwetu hilo ni kosa kubwa,” amesema Magomi.

Katika hatua nyingine Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga, amesema Jeshi hilo katika msako huo limefanikiwa kukamata mafuta lita 780 aina ya dizeli ambayo yameibwa kwenye mradi wa ujenzi wa Reli ya kisasa (SGR) pamoja na Pikipiki tatu ambazo zilikuwa zikitumia katika wizi huo wa mafuta.

Ametaja vitu vingine vya wizi ambavyo wamevikamata kuwa ni milango Tisa ya chuma, mabomba ya alama za usalama barabarani, milango mitano ya mbao, mizani ya kupimia uzito, mashine ya kutoboa miamba, Godoro moja, viti vinne vya Plastiki, Ngoma moja ya shule na Magitaa mawili, vifaa tiba, na mashine mbili za kamali.

Ameemdelea kuvitaja vitu vya wizi ambavyo wamekamata kuwa ni Subwoofer Mbili, Feni moja, mtungi mmoja wa gesi na pia ameokota pikipiki mbili, huku akibainisha kuwa wamekamata Bangi Kete 31, pamoja na kukamata waganga wa Jadi watatu wakiwa na vifaa vya kupigia Ramlichonganishi ambavyo husababisha mauaji ya kikatili.

Amesema kwa upande wa Mahakama jumla ya kesi mbalimbali 16 zilipata mafanikio kwamba kesi Nane za makosa ya wizi zilihukumiwa na wahusika kufungwa miaka mitatu, kesi Nne za wazazi kutopeleka shule watoto, kuwa wazazi walipigwa faini ya sh.100,000, na Kesi moja ya ushirikina mhusika alikwenda Jela miezi sita, pamoja na upatikanaji wa mali wizi ilihukumiwa kulipa faini Sh. 300,000.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Janeth Magomi akionesha vitu vya wizi ambavyo wamevikamata yakiwamo na Mafuta lita 780 kutoka mradi wa ujenzi wa Reli ya kisasa SGR.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Janeth Magomi akionesha vifaa Tiba ambavyo vimeibwa kwenye Hospitali.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Janeth Magomi akionesha vifaa vya uganga ambavyo vimekuwa vikitumika kupiga Ramli Chonganishi na kusababisha mauaji ya kikatili yakiwamo ya ukataji mapanga.

Vifaa vya uganga vya kupiga Ramli Chonganishi.

Pikipiki zilizokamatwa zikitumika katika wizi wa mafuta Mradi wa SGR. na nyingine Mbili kuokotwa.

Vitu mbalimbali vilivyokamatwa zikiwa vimeibwa

Vitu mbalimbali vilivyokamatwa zikiwa vimeibwa.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464