Maduka siyo halisi ya Kishapu ambayo yamefungwa
Na Marco Maduhu, KISHAPU
Wafanyabiashara wilayani Kishapu wamelalamikia Maofisa Biashara wa halmashauri hiyo kutumia mabavu kudai kodi, na kuwafungia biashara zao bila utaratibu, huku wakiwazuia wasizime majokofu, kuchukua simu kwa waliozisahau ndani wala fedha za mauzo na kuwatolea lugha zisizo na staha.
Wamepaza sauti hizo leo wakati wakizungumza na vyombo vya habari kulalamikia matumizi ya nguvu kudai kodi, huku wakifungiwa vitu vyao ndani bila hata ya kuzima vifaa ambavyo vinatumia umeme, hali ambayo ni hatari kuweza kutokea shorti ya umeme na kuleta maafa.
Mmoja wa wafanyabiashara hao ambaye ameomba (jina lake lihifadhiwe), amesema wao hawajakataa kuwa wanadaiwa Kodi, lakini wanasikitishwa na matumizi ya nguvu huku wakizuiwa wasichukue hela za mauzo, simu wala kuzima majokofu hali ambayo inaweza kusabisha chupa kuvunjika na hata kutokea shorti ya umeme na kusababisha maafa.
“Leo majira ya saa 4 asubuhi wamekuja maaofisa wa Serikali kutoka Halmashauri kudai Kodi, ni kweli tunadaiwa na hatujakataa kulipa lakini utaratibu ambao wamekuja nao siyo mzuri wanatumia mabavu, kitendo ambacho ni kinyume na Tamko la Rais Samia la kudai Kodi kwa utaratibu,”amesema Mfanyabiashara huyo.
“Yani wanafungia hovyo biashara harafu wanazuia usikuchukue hata hela za mauzo wala simu kama imeicha ndani na hakuna kuzima Jokofu na wakati lina soda ndani je chupa zikipasuka itakuwaje, na wilaya hii ya Kishapu inatabia ya kudai kodi kwa mabavu tuna muomba Rais aimulike Kishapu,”ameongeza.
Aidha, amesema baadhi yao hawana malimbikizo ya Kodi na wanalipa Kodi hawajagoma, ila wanasikitika na kuharasiwa namna hiyo kama wahalifu.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu Emmanuel Johnsoni alipopigiwa simu kuzumgumzia Malalamiko hayo amekanusha kuwa hakuna matumzi ya nguvu yaliyotumika kudai Kodi.
Amesema tayari ameshaagiza maofisa wake kufungua dirisha la malalamiko la wafanyabiashara na kwamba wamefike kwenye dirisha hilo kutoa malalamiko yao na kuandika maelezo kuwa watalipa lini kodi.
"Tumechoka halmashauri ya wilaya ya Kishapu kuwa wa mwisho kwenye ukusanyaji wa mapato, na hakuna ambaye ameonewa tangu mwezi Julai mwaka jana hadi leo hawajalipa Kodi, walipe Kodi ili zipatikane fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo, mfano mwaka wa fedha 2023/2024 tumetenga mapato ya ndani kujenga kituo cha afya Mwamalasa sasa fedha zitapatikana wapi, na nyie waandishi toeni elimu wafanyabishara walipe kodi,"amesema Johnson.