Kiasi cha Sh4.5 bilioni kimetumika kufanya uwekezaji wa ujenzi, miundombinu na vifaa tiba vilivyotumika kuanzisha Kituo cha Huduma Pandikizi (IVF) cha Hubert Kairuki.
Kituo hicho cha kutoa huduma hiyo kipo Bunju A jijini Dar es Salaam kikiwa na uwezo wa kufanya upandikizaji kwa watu 1,000 kwa mwaka.
Akizungumza leo Februari 6, 2023 wakati wa uzinduzi wa kituo hicho, Mtendaji Mkuu wa Hubert Kairuki Hospital Green IVF, Dk Clementina Kairuki amesema kituo hicho kinalenga kuhakikisha huduma bora za uzazi pandikizi zinawafikia Watanzania walio wengi.
Lengo lingine la uanzishwaji wa kituo hicho ni kufanya tafiti zitakazoweza kubaini ukubwa wa tatizo la ugumba kitaifa na kuboresha matibabu.
Amesema tayari watu 600 wamejitokeza kutafuta huduma hiyo tangu kuanzishwa kwake na walipochunguzwa ilibainika 45 kati yao walionekana kuhitaji huduma hiyo ya upandikizaji na tayari wameshapandikizwa.
Kuhusu gharama za huduma hiyo, Dk Clementina amesema inagharimu kati ya Sh13 milioni hadi Sh15 milioni kuwezesha mtu kufanyiwa upandikizaji na hiyo inachangiwa na kutegemea vifaa na dawa kutoka nje ya nchi.
“Kati ya hawa 45 tayari 35 wameshapata ujauzito, kwa hiyo tunakwenda vizuri maana huduma hii matokeo yake yanaweza yasiwe kwa asilimia 100 lakini kwa kuwa sisi ndiyo tumeanza na tumepata matokeo hayo inaleta matumaini,” amesema Dk Clementina.
SOMA HAPA ZAIDI CHANZO MWANANCHI.