Wanafunzi wa darasa la awali shule ya msingi Puni
Na
Kareny Masasy Shinyanga
WAZAZI wa kijiji cha Puni halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wamedai msimu wa mavuno wako tayari kuchangia chakula shuleni bila wasiwasi wowote.
Wakazi wa kijiji hicho Somson Jeremiah na Suzana Gawinde wanasema kwa mara ya kwanza walipewa Elimu juu ya faida ya wanafunzi kupata chakula shuleni mwaka 2019 kutoka shirika la kimataifa la Save the Children.
Jeremiah anasema shirika hilo lilihamasisha wazazi wa shule ya msingi Puni hasa kwa wanafunzi wa darasa la awali na kwanza kupata angalau uji nyakati za asubuhi.
“Tulishiriki ndani ya mwaka mmoja kuchangia upatikanaji wa uji kwa wanafunzi na badaye ikasitishwa ghafla lakini tungetekeleza ingezoeleka kwa wazazi sasa wanakumbushwa walishasahau”.anasema Jeremiah.
Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Puni Leonard Kawili anasema shule hiyo ilianzishwa mwaka 1976 ina wanafunzi 610 ambapo darasa la awali wako 69 na darasa la kwanza wako 93.
“Mwaka 2019 wazazi walihamasishwa kuchangia chakula shuleni lakini walianzia na unywaji uji kwa darasa la awali na kwanza ili waweze kucheza na kusikia vizuri darasani”.anasema Kawili.
Mwalimu Kawili anasema sasa hivi hawapati chakula shuleni ila wazazi walitoa ahadi kipindi cha Mavuno wako tayari kuchagia Mahindi ili kusaga nakupata unga wa uji.
Mwalimu Kawili anasema Siku moja mtoto wa darasa la kwanza alikutwa amelala njiani hana nguvu mwalimu alipofuatilia hadi kwa wazazi wake ikabainika anatoka kwenye familia duni na hakula usiku chakula chochote nyumbani.
Mwalimu Kawili anasema upatikanaji wa chakula shuleni unasaidia hata kwa watoto wanaotoka kwenye familia duni kupata chakula na kupenda shule kuondoakana na utoro wa rejareja.
Katibu wa jeshi la sungusungu kutoka kijiji cha Puni Abel Mafumka anasema wazazi watakapo vuna watapeleka mahindi hayo kwenye uongozi wa sungusungu na wao wataikabidhi shule.
“Mikakati tuliyoiweka nikuhakikisha kila mzazi mwenye mwanafunzi anachangia debe la mahindi kwa kulileta kwenye uongozi wa sungusungu” anasema Mafumka.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Dodoma Maige Robert anasema wazazi wamekubaliana kuchangia debe moja moja la mahindi shuleni kila mwenye mtoto pindi watakapo vuna.
Maige anasema kitongoji hicho kina wakazi zaidi ya 200 na shughuli zao kuu ni ufugaji na kilimo na suala la elimu kwao sio kipaumbele hawana mwamko.
“Wanafunzi hawapati chakula shuleni walihamasishwa kwenye mkutano wa hadhara wakadai wataanza kuchangia msimu wa mavuno”anasema Robert.
Kaimu mtendaji wa kijiji cha Puni ambaye ni ofisa maendeleo ya jamii wa kata Veronika George anasema uchangiaji wa chakula shuleni wazazi wanakosa utayari mpaka kupitia jeshi la sungusungu.
“Kijiji cha Puni kina vitongoji 10,kaya 319 na idadi ya watu kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 ni 1595 ambapo wanaume 638 na wanawake 957”anasema George.
Mtendaji wa kata ya Puni Fumbuka Mathias anasema kata hiyo ina shule tatu za msingi na zote watoto hawapati chakula shuleni baada ya mkutano wa hadhara wamekubali kuchangia msimu wa mavuno.
Diwani wa kata ya Puni Heke Salum anasema alifanya mkutano kwenye kila kijiji nakuahidi kila shule kuchangia gunia moja la mahindi msimu wa mavuno.
Ofisa lishe wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Said Mankilago anasema mwanafunzi akinywa uji wenye sukari inatosha kumpatia nguvu kuliko kukaa bila kula muda mrefu.
“Kwani tunasisitiza angalau wapate uji shuleni kwani utatumika unga ambao ni kundi la vyakula vya wanga na sukari itawapa virutubisho mwilini”anasema Mankilago.
Mankilago anasema ili chakula kipatikane wametumia jeshi la sungusungu kuhamaisha na kuwekeana sheria za uchangiaji kwani jamii bado haina uelewa juu ya lishe.
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Nice Munisy anasema kuna shule za msingi 139 na upatikanaji wa chakula shuleni umefikia asilimia 89.
Munisy amewataka madiwani kwenye maeneo yao kuhamaisha wazazi kuchangia chakula shuleni .
Ofisa Elimu mkoa wa Shinyanga Dafroza Ndalichako anasema kuna shule za msingi za serikali 603 kati ya hizo shule 293 sawa na asilimia 48.5 ndiyo zinatoa chakula shuleni .
“ Jumla ya wanafunzi 545,339 kwa mkoa mzima wa shule za msingi na shule 310 hazitoi chakula shuleni mpaka sasa hivyo jitihada zinafanywa na wazazi kuhakikisha watoto wanapata chakula”anasema Ndalichako.
Katika program jumuishi ya Taifa ya Malezi ,Makunzi na maendeleo ya Awali ya Mtoto ( PJT-MMMAM) 2021/22 hadi 2025/26 inaeleza afua za lishe hazishughulikii kwenye elimu ya madarasa ya awali na kwanza kwa shule za msingi.
Maeneo ambayo yameonekana kuna program za lishe shuleni nikutokana na juhudi za wadau zinazotokana na ubunifu wao kama sehemu ya majaribio ya program shuleni.
Aidha lishe hiyo imeonekana ni uji ambayo haifikii kiwango cha vyakula bora vyenye mchanganyiko ambapo Taasisi ya chakula na lishe nchini (TFNC) inaandaa toleo la kwanza la muongozo wa kitaifa wa utoaji wa huduma ya chakula na lishe kwa wanafunzi elimu ya msingi.