
Suzy Luhende, Shinyanga Shinyanga blog
Mwenyekiti wa jumuia ya wazazi CCM mkoa wa Shinyanga John Siagi amewataka viongozi wa Chama Cha Mapinduzi CCM na jumuia zake ngazi ya mabalozi, matawi na kata kufanya vikao mara kwa mara ili kuboresha Chama na jumuia zake.
Hayo ameyasema jana wakati akizungumza kwenye kikao na wajumbe wa halmashauri kuu ngazi ya kata pamoja na jumuia zake na viongozi wa matawi katika kata ya Mwendakulima wilayani Kahama mkoani Shinyanga,ambapo pia akiwa na viongozi hao alifanikiwa kutembelea kituo cha afya cha Mwendakulima na kuwajulia hali wanawake wajawazito, wazazi na wagonjwa.
Siagi ambaye aliambatana na viongozi mbalimbali wa jumuiya ya wazazi mkoa akiwemo katibu wa wazazi Rejina Ndulu na Mjumbe wa baraza la wazazi Taifa Edwin Nyakanyenge na mjumbe wa baraza mkoa Agnes Kahabi aliwasisitiza viongozi ngazi ya kata wawe wanafanya vikao mara kwa mara ili kuimalisha Chama na jumuia zake kuanzia ngazi ya mabalozi, huku wakihamasisha wananchi kujiunga na Chama Cha Mapinduzi.
"Ndugu zangu Jumuia ya Wazazi, UWT, na Chama fanyeni vikao na kwenye vikao hivyo mtatue changamoto zilizopo kwa wananchi msiwe wavivu, kwa sababu Chama ndio kinasimamia serikali na miradi mbalimbali na kutetea wanyonge waweze kutendewa haki, hivyo tatueni migogoro kwa wananchi," amesema Siagi.
" Nawaomba ndugu zangu msigeuke kuwa kero kwa wananchi badala yake muwe sehemu ya kutatua kero, kwani Chama chetu ni chama cha amani, hivyo nasisitiza ushirikiano, upendo na mshikamano, shaulianeni kwa pamoja ili kufanya vitu vizuri," amesisitiza Mwenyekiti Siagi.
Aidha Siagi ameitaka jumuia ya wazazi kupanga muda wa kutoa elimu Mashuleni na kuwasikiliza watoto ili kujua wanachangamoto gani waweze kusaidiwa, ikiwa ni pamoja na kufanya Makongamano ya kukemea ushoga ubakaji na ulawiti.
" Pia niwaombe viongozi wenzangu kwamba tunapofanya siasa tunatakiwa tuwe wabunifu wa kufanya miradi mbalimbali, ili kuweza kujikwamua kiuchumi, kwani siasa yetu inaendana na miradi,pia wahamasisheni kina mama na vijana wachukue kadi za jumuia ya wazazi na za Chama ili waweze kujiunga vikundi wapate mikopo ya halmashauri wafanye miradi mbalimbali ya kujiongezea kipato,"amesema Siagi.
Hata hivyo Siagi alifanikiwa kugawa kadi za jumuiya na chama kwa wanachama zaidi ya 50 wa kata ya Mwendakulima ambao nao waliahidi kukitumikia Chama Cha Mapinduzi kwa uaminifu wote, kwa sababu ni chama kinachojali wanyonge.
Baadhi ya wazazi, wajawazito na wagonjwa Joseph Philipo na Agnes Piter walikishukuru Chama Cha Mapinduzi na Jumuiya zake kwa kuwakumbuka na kuwapelekea zawadi mbalimbali zikiwemo sabuni za kufulia, Mafuta ya kupaka, na Juice, ambazo zitawasaidia kwa wakati watakao kuwepo hospitalini hapo.
Kwa upande wake Katibu wa Jumuiya ya wazazi mkoa wa Shinyanga Rejina Ndulu ambaye aliambatana na mwenyekiti amewataka waendelee kushirikiana kwa pamoja ili kuhakikisha Jumuiya ya wazazi inaimarika zaidi.



Diwani wa kata ya Mwendakulima akizungumza katika kikao hocho


Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi mkoa wa Shinyanga John Siagi akikabidhi kadi ya Chama kwa mwananchi wa kata ya Mwendakulima


Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi John Siagi akitoa maelekezo kwa kaimu mganga mkuu wa kituo cha afya Mwendakulima


Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi mkoa wa Shinyanga John Siagi akikabidhi kadi ya Chama kwa mwananchi wa kata ya Mwendakulima



Katibu wa Jumuiya ya wazazi mkoa akimpongeza mwalimu wa shule ya msingi Mwendakulimakwa kupokea kadi ya Jumuia ya wazazi










Kikao kikiendelea katika kata ya Mwendakulima