Mwenyekiti wa Umoja wa wanawake UWT wilaya ya Shinyanga Rehema Namanilo akizungumza baada kusalimia wanawake wafungwa katika gereza la Shinyanga
Suzy Luhende, Shinyanga blog
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake UWT CCM Mkoa wa Shinyanga Grace Samweli amewahimiza wanawake Mkoani Shinyanga kuwa mstari wa mbele katika kuzingatia malezi kwa watoto, kuliko kuwa bize na kukimbizana na mikopo umiza.
Agizo hilo amelitoa leo baada ya kufanya matembezi ya mtaa kwa mtaa ya kukemea vitendo vya ukatili wa kijinsia yaliyoambatana na kutoa msaada kwa gereza la wanawake lililopo wilayani Shinyanga katika siku za kuelekea maadhimisho ya siku ya mwanamke duniani ifikapo machi 8 mwaka huu yaliyoandaliwa na UWT Wilaya ya Shinyanga mjini.
Grace amesema wanawake wengi wamepoteza mwelekeo kila wanapoamka wanakimbizana na marejesho tu, huku wakisahau malezi kwa watoto wao na kusahau majukumu yao kwa wenza wao, ndiyo maana matukio ya ukatili yanazidi kuongezeka.
"Hali ya ukatili wa kijinsia ni mbaya sana kwa mkoa wa Shinyanga, tuangalie wapi tunafeli tuweze kujirekebisha, kwani mpaka sasa mkoa wa Shinyanga tunaongoza kwa ukatili wamama tunaondoka asubuhi na kurudi usiku kwa sababu mikopo tunaizidisha jamani, ndiyo maana unakuta wababa wanatoka na watoto wao kwa sababu wewe mama haushikiki, kuanzia leo tubadilike turudi kwenye maadili tufanye wajibu wetu"amesema Grace.
Mjumbe wa baraza la UWT Taifa Christina Gule amewapongeza wanawake wa UWT wilaya kwa kitendo walichokifanya cha kwenda kuwajulia hali wanawake gerezani na kuwapa msaada wa vitu mbalimbali zikiwemo sabuni za kufulia taulo za kike, mafuta na dawa ya meno, mmefanya jambo la kimungu sana.
"Kutokana na takwimu kuongezeka za matukio ya ukatili tunalaani vikali matukio ya kikatili, kwani kina mama wengi wapo gerezani kwa sababu ya kujitetea matendo haya yanatakiwa yakome kabisa, tukiwa tunalaani tuangalie tabia zetu, tuache tabia mbaya tumruhusu Mungu atawale maishani mwetu wanawake tubadilike tuwe na upendo na hofu ya Mungu,"amesema Gule.
Kwa upande wake katibu wa UWT Mkoa wa Shinyanga amesema kila aliyeguswa anapata thawabu, hiyo ni sadaka nzuri kwa mwenyezi Mungu, lakini amewasihi wanawake wafundishe maadili mema watoto ili wasiendelee kufanyiwa ukatili na wanaume wasio wazuri ambao hawana maadili ya kimungu.
Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Shinyanga Rehema Namanilo aliwashukuru wanawake wote waliojitokeza kwenye matembezi ya kupinga ukatili wa kijinsia na kuwatembelea wanawake gerezani, pia amekemea kitendo cha wanaume wanaoendelea kufanya ukatili kwa watoto wao na kwa watoto wa ndugu zao.
Hata hivyo baada ya kutoa msaada kwa wanawake gerezani Wanawake UWT wilaya walipewa elimu na afisa kutoka dawati la jinsia na watoto wilaya ya Shinyanga mjini Inspector Jane Mwazembe ambaye amesema matukio ya ulawiti yamekuwa mengi kwa wilaya ya Shinyanga na kuwataka wazazi kuwafuatilia watoto wa kiume na kujenga ukaribu nao.
"Pia tuwe makini tunapokaribisha wageni wetu tusiwaache walale na watoto wetu afadhali tuwatafutie sehemu ya kulala kuliko kuwachanganya kila mmoja awe. makini,na tutoe taarifa za ukatili tunapoona wanawake ama watoto wanafanyiwa ukatili, na tusaidie kutoa elimu katika maeneo yetu ili wawe wanatoa ushahidi pindi yanapotokea matukio ya ukatili,"amesema Mwazembe.
Baadhi ya wajumbe akiwemo Mery Makamba ameshauri kuwa wazazi wasiachie watoto simu kwani ndiyo zimekuwa zikisababisha shida kwa watoto, na kina mama wapunguze ubize wawalinde watoto wao,ili kupunguza matukio ya kiukatili na ekimu itolewe kuanzia ngazi ya vijiji kwa sababu watu wengi hawana elimu ya kutoa taarifa hawaelewi ni wapi wapeleke taarifa.
Kwa upande wake mkuu wa gereza msaidizi Abell Gwambasa amewashukuru wanawake UWT wilaya ya Shinyanga mjini kwa kuwakumbuka wanake gerezani ambao wapo 17, hivyo amewaomba waendelee kuwa na moyo huo na wadau wengine wakiguswa waje wanakaribishwa.


















Wanawake wa UWT Wilaya ya Shinyanga wakiwa kwenye maandamano wakielekea magereza kwa ajili ya kuwasalimia wanawake gerezani

Wanawake wa UWT Wilaya ya Shinyanga wakiwa kwenye maandamano wakielekea magereza kwa ajili ya kuwasalimia wanawake gerezani







