RAS SHINYANGA AWATAKA WAKURUGENZI KUSIMAMIA AFUA ZA UGAVI WA BIDHAA ZA AFYA, NA KUWACHUKULIA HATUA KALI WATUMISHI WATAKAOBAINIKA WANAIBA DAWA ZA SERIKALI, IKIBIDI KUWAFUKUZA KAZI KABISA



Suzy Luhende, Shinyanga Press Club

Katibu Tawala wa mkoa wa Shinyanga Sizza Tumbo amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri za mkoa wa Shinyanga kusimamia kikamilifu afua mbalimbali za Mfumo wa Ugavi wa Bidhaa za Afya ikiwemo kufanya Medicine Audit mara kwa mara katika vituo vya kutolea huduma, kwa ajili ya kupunguza changamoto zinazotokana na usimamizi mbovu wa bidhaa hizo ili kuondokana na wizi wa madawa.

Hayo ameyasema leo wakati akifungua mafunzo ya siku tatu  kwa wakurugenzi wa halmashauri, waganga wakuu wa wilaya, wafamasia na maafisa ugavi wa vifaa vya afya kutoka halmashauri zote za mkoa wa Shinyanga, ailiyofsnyika katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa mkoa Shinyanga, ambapo lengo la mafunzo hayo ilikuwa ni kupata wawezeshaji wa Mkoa na Halmashauri (T.O.Ts) wa Mfumo wa Mshitiri, ili kuwawezesha kusimamia kikamilifu madawa.

Tumbo amesema kabla ya mfumo  wa Mshitiri dawa zilikuwa zikiibiwa sana na zingine kupelekwa kwenye majumba ya watu, lakini kwa sasa mfumo umeboreshwa wizi hautakuwepo tena na atakayepatikana anafanya wizi katika mfumo huo achukuliwe hatua kali hata ikibidi afukuzwe kazi.

"Mlioko kwenye mafunzo haya kila mmoja akatimize wajibu wake, niwaombe mkasimamie ipasavyo na mkahakikishe hizo dawa haziibiwi ili ziweze kufika na kutumika kwenye vituo husika,na mkasimamie ukusanyaji wa mapato katika vituo vya kutolea huduma za Afya, ili viweze kulipa Washitiri kwa wakati mara baada ya kupokea shehena ya bidhaa, kuepushe madeni yasiyo ya lazima,"amesema Tumbo.

"Unakuta mtu analipwa mshahara halafu anaiba, hivyo hao watumishi wanatakiwa mkawape elimu na sababu kubwa ya kuleta mfumo huu ni kuondokana na wizi wa madawa, naombeni tubadilike tuwe wazalendo atakaebainika anaiba dawa za serikali achukuliwe hatua kali ikibidi afukuzwe kazi kabisa,"ameongeza Tumbo.

Aidha amesema kwa kutambua hilo, Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, imekuwa ikitekeleza afua mbalimbali ili kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa za afya unakuwa asilimia 100% ikiwemo Mfumo wa Mshitiri na uwepo wa mfumo wa Mshitiri ni utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 kama ilivyoainishwa katika sura ya tatu sehemu ya 18 (i) na (aa).

Kwa upande wake mjumbe wa timu ya uratibu ya mfumo wa mshitiri kutoka ofisi ya Rais Tawala za mikoa na serikali za mikoa  (Tamisemi) Amiri Mhando amesema mfumo huo utarahisisha kupatikana kwa huduma za kupata vifaa vya afya kwa wakati na utapunguza kuondoa upotevu wa dawa.

"Na hii itasaidia kutunza kumbukumbu kwa sababu ya kutumia njia za kielectonic tofauti na awali wahusika  walikuwa wakisahau kuhifadhi, pia njia hiyo itasaidia kupunguza hoja za ukaguzi na italeta ufanisi kwa kuondoa tatizo la upungufu wa vifaa vya afya,vifaa vitafika kwenye vituo kwa wakati,"amesema Mhando.

Naye mfamasia kutoka wilaya ya Ushetu Alphonce Malunde amesema mfumo huo utarahisisha upatikanaji wa dawa na itarahisisha utunzaji wa kumbukumbu,na Balungi Samson mfamasia kutoka wilaya ya Kishapu amesema elimu hiyo wataitumia kwenda kutoa kwa wahudumu wa afya ili kuondokana na changamoto iliyokuwepo ya mawasiliano ambayo ilikuwa ikitumika kwa muda mrefu.
Mjumbe wa timu ya uratibu ya mfumo wa mshitiri kutoka ofisi ya Rais Tawala za mikoa na serikali za mikoa (Tamisemi) Amiri Mhando akitoa maelekezo kwenye mafunzo hayoWafamasia na wakurugenzi mkoa wa Shinyanga wakiwa kwenye mafuzo
Mafunzo yakiendelea
Wakiendelea kupata maelekezo




Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464