BIASHARA SACCOS WAWAKUMBUKA WATOTO WENYE MAHITAJI MAALUMU



Mwenyekiti wa Biashara Saccos Shinyanga, Fue Mrindoko (mwenye kofia) akikabidhi msaada kwa watoto wenye mahitaji maalum katika Shule ya msingi Buhangija Jumuishi. Kushoto ni meneja wa Biashara Saccos, Damas Leo na wa kwanza kulia ni mlezi wa watoto hao, Frola Kilomole.

Na Suleiman Abeid, Shinyanga blog

MWENYEKITI wa Chama cha Akiba na Mikopo – Biashara SACCOS cha mjini Shinyanga, Fue Mrindoko ametoa wito kwa wazazi na walezi wote wenye watoto wanaosoma na kulelewa katika shule ya msingi Buhangija Jumuishi kuwatembelea na kuwajulia hali watoto wao.

Mrindoko ametoa wito huo wakati akikakabidhi msaada kwa watoto wenye mahitaji maalum wanaosoma kwenye shule ya msingi Buhangija Jumuishi ambao umetolewa na uongozi wa Bodi ya Biashara SACCOS Shinyanga.

Amesema pamoja na Serikali kuweka mpango mzuri wa malezi ya watoto wenye mahitaji maalum hasa wale wenye Ualbino lakini bado wapo wazazi na walezi ambao wameigeuza fursa hiyo kuwa “fimbo” ya kuwaadhibu watoto wao kwa kuamua kuwatekeleza shuleni hapo.

“Tumekuja hapa kuwatembelea watoto wetu hawa wenye mahitaji maalum, wakiwemo wenye ualbino, viziwi na wale wasioona ili kuwapatia msaada utakaowasaidia katika mahitaji yao muhimu ya kila siku ikiwemo sabuni za kufulia, miswaki, dawa za meno na viatu,”“Watoto hawa ni sehemu ya jamii ya watanzania, hivyo wanahitaji kila mara kutembelewa na kupewa misaada mbalimbali ili waweze kuishi kama wanavyoishi watoto wenzao wasiokuwa na mahitaji maalum, na niwaombe wazazi wenzantu, tusikigeuze kituo hicho kama kituo cha kuwatelekeza watoto hawa,” ameeleza Mrindoko.

Mrindoko ambaye mbali ya kuwa mwenyekiti wa Biashara Saccos pia ni mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Shinyanga mjini ametoa wito kwa wazazi ama walezi ambao wamewatelekeza watoto wao katika shule hiyo ya Buhangija kujitokeza ili kuwatembelea na kuwachukua vipindi vya likizo ili na wao wajihisi wana wazazi.

“Nitoe wito kwa wazazi wote wenye watoto kwenye shule hii ambao wamewatelekeza kipindi kirefu watoto wao waje wawatembelee na vipindi vya likizo wawaijie wakapumzike majumbani, hii watajiona wako sawa na wengine, vinginevyo kuwatelekeza hapa ni sawa na kuwatendea ukatili,” ameeleza Mrindoko.

Kwa upande wake mmoja wa walezi wa watoto kwenye shule hiyo, Frola Kilomole amewashukuru wajumbe wa Bodi ya Biashara Saccos kwa msaada ambao wameutoa na kuwaomba waendelee na moyo huo kila mara kwa vile watoto hao wana mahitaji mengi.

Naye Meneja wa Biashara Saccos, Damas Leo amesema pamoja na majukumu mengine ya Saccos yao lakini pia wana wajibu wa kurejesha kwa jamii sehemu ya kile wanachokipata katika shughuli zao za utoaji mikopo.

“Tumekaa na kuona ni vyema tuikumbuke pia jamii yetu kwa kurejesha kile kidogo tunachokipata, na katika sheria zetu za ushirika kuna kitu kinaitwa, misingi, kwenye hiyo misingi kuna msingi namba saba wa kujali jamii, kwa hiyo imekuwa ni furaha kwetu kujumuika pamoja nanyi tukasema na sisi kwa sehemu yetu angalao kwa kiasi kidogo tuweze kuwapunguzia uhitaji, mungu ametujalia hiki kidogo tulichonacho ili tuweze kuwapatia watoto wetu wenye mahitaji maalum mnaosoma hapa shule ya msingi Buhangija Jumuishi,” ameeleza Damas.

Mwenyekiti wa Ushirika wa Biashara Saccos Shinyanga, Fue Mrindoko.

Mmoja wa walezi wa watoto wenye mahitaji maalum katika shule ya msingi Buhangija Jumuishi Manispaa ya Shinyanga, Frola Kilomole.
Mwenyekiti wa Biashara Saccos Shinyanga, Fue Mrindoko (mwenye kofia) akikabidhi msaada kwa watoto wenye mahitaji maalum katika Shule ya msingi Buhangija Jumuishi. Kushoto ni meneja wa Biashara Saccos, Damas Leo.

Wajumbe wa Bodi ya Ushirika Biashara Saccos Shinyanga, kutoka kushoto ni Meneja wa Biashara Saccos, Damas Leo, Fue Mrindoko na mjumbe Peter Subi.
Mwenyekiti wa Ushirika wa Biashara Saccos (mwenye kofia) Fue Mrindoko na mjumbe wa Bodi ya ushirika huo (mwenye koti la bluu) wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watoto wenye mahitaji maalum baada ya kuwakabidhi msaada.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464