Baraza la Wazee wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kwa kauli moja limewapongeza Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga Mhe. Elias Masumbuko kwa niaba ya Waheshimiwa Madiwani wote na Ndg. Jomaary Satura kwa niaba ya watumishi wote wa Manispaa kwa utendaji kazi wao bora katika nyanja mbalimbali ikiwamo utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Akisoma baadhi ya mafanikio kwa uongozi Katibu wa Baraza, mzee Laurent Kashindye amesema kwamba ni pamoja na kupandisha ukusanyaji wa mapato mara mbili zaidi ya awali, kuimarisha nidhamu kwa watumishi na katika matumizi ya fedha za Serikali, uboreshaji wa miundombinu ya ufanyaji biashara na uwezeshaji wananchi kiuchumi, elimu, afya pamoja na kuboresha mazingira na upendeshaji wa mji wa Shinyanga.
Hayo yamesemwa leo terehe 28 Aprili, 2023 wakati Katibu wa Baraza la Wazee Ndg. Laurent Kashindye akisoma Risala ya Wazee kwa wajumbe wa baraza na uongozi wa Manispaa wakati wa mkutano huo ambao pamoja na wajumbe wake lakini pia alikuwepo Mwenyekiti wa Wazee Mkoa wa Shinyanga mzee Faustine Sengerema.
Akifungua Mkutano huo na kutoa salamu za wazee, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Manispaa mzee Stephano Tano amesema kwamba Baraza la Wazee linaridhishwa na kufurahishwa sana na mwenendo wa utumishi wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Ndg. Jomaary Satura na wasaidizi wake wote kwa namna ambavyo wanaiheshimisha Manispaa kitaifa, katika ubunifu wake na utekelezaji wa mipango yao kisasa zaidi, na Mstahiki Meya Mhe. Elias Masumbuko na Waheshimiwa Madiwani kwa usimamizi ulio bora kabisa kwa Menejimenti hata sasa wameifanya Manispaa kuwa ya kuigwa na Halmashauri nyingine katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati.
"Kwa kauli moja tunawapongeza ninyi viongozi wa Manispaa kwa namna ambavyo mmeweza kutekeleza shughuli zenu za kuwahudumia wananchi, kuanzisha, kusimamia na kuboresha miradi ya kimkakati kama ambavyo taatifa yetu imeeleza hongereni sana," amesema Mzee Tano.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Mkoa wa Shinyanga mzee Faustine Sengerema amesema kuwa, pamoja na pongezi hizo kwa Manispaa lakini akasisitiza kuwa kuzinduliwa rasmi kwa Baraza hilo kunakwenda kuimarisha na kutambua thamani ya wazee kwa Manispaa kwakuwa sasa wataanza kushirikishwa rasmi katika ngazi mbalimbali za maamuzi na vikao rasmi kama vile Baraza la Madiwani, Kamati za Maendeleo za Kata na vikao rasmi vya kila mwaka ambavyo vinatamkwa katika muongozo wa uanzishwaji wa mabaraza ya wazee nchini.
Akitoa salamu kwa niaba ya Manispaa ya Shinyanga Mkurugenzi hiyo Jomaary Satura amesema katika utekelezaji wake wa shughuli za kila siku, Manispaa inaheshimu sana, inatambua na kuthamini michango na uwepo wa wazee katika Manispaa huku akiwaomba ushirikiano zaidi na kwamba milango ipo wazi kwa Manispaa na wanakaribishwa wakati wowote.
Aidha Mstahiki Meya Mhe. Masumbuko amewaeleza wazee kuwa yeye na Baraza zima la Manispaa wanapokea ushauri wote uliotolewa, wataufanyia kazi na kwamba waheshimiwa madiwani wanawategemea sana wazee katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.