Suzy Luhende,Shinyanga, blog
Mkazi wa Kijiji cha Ikoma Kata ya Itilima Halmashauri ya Kishapu Mkoani Shinyanga, mwenye umri wa miaka 26 amepigwa viboko hadharani na jeshi la jadi sungusungu kwenye uwanja uliopo katika kijiji hicho na zaidi ya sungu sungu 30 baada ya kutuhumiwa kuiba Sh 420,000 za mteja wake na hali iliyosababisha kulazwa hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga.
Tukio hilo lilitokea April 14 mwaka huu katika Kijiji cha Ikoma Kata ya Itilima Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga,ambapo mwanamke huyo huyo anayefahamika kwa jina la Manka Mushi(26) alikuwa akifanya kazi baa na nyumba ya kulala wageni kijijini humo ndipo mwanaume mmoja anayefahanika kwa jina la Julias Marimo ambaye alikuwa akimtaka kimapenzi na kumkataa alimuomba ampelekee shuka chumbani.
Manka akisimulia mkasa huo uliomkuta amesema ilikuwa majira ya saa sita usiku alipopeleka shuka baada ya mteja kuomba, ndipo alimkaba koo akimtaka kurudisha fedha hizo ambazo anahisi alichukuwa alikataa kuhusika na wizi huo na kumwambia kwa kuwa alimkataa atamtambua na alianza kupiga kelele za kuomba msaada na kufanikiwa kutoka ndani.
"Usiku huo huo mteja alikuja kugonga tulipokuwa akaomba shuka niliinuka kumpelekea, lakini cha kusikitisha baada ya kufikisha shuka alinigeuka akasema nimeiba hela alinipiga sana akiniambia kwa nini nilimkataa atanionyesha mimi nilimwambia sijachukuwa hela na asubuhi akaenda kwa kamanda wa sungusungu wa Kijiji nikaitwa”amesema Manka.
Kufuatia hatua hiyo niliambiwa na kamanda wa sungusungu twende uwanjani na baada ya kufika nilikuwa mwanamke peke yangu nikaambiwa ni lale chini katikati ya wanaume zaidi ya 30 ukaletwa mzigo wa fimbo wakaanza kunipiga viboko kwa zamu nikijaribu kuinuka wengine wanapiga mgongoni na kichwani.
Amesema aliwapa namba ya mama yake mzazi ambaye anaishi Jijini Arusha walimpigia na kuzungumza naye kisha kumtaka atume hela lakini aliwaomba wampeleke polisi, na baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya walimpeleka ofisi ya Kata kwa ajili ya kutoa maelezo, lakini walikataa kumpokea.
Amesema anamshukuru mungu kwa sasa anaendelea vizuri tofauti na awali, ambapo sehemu ya makalio na mgongoni kulikuwa kumejaa vidonda,ambapo ameiomba serikali kuchukuwa hatua kali kwa sungusungu waliomfanyia kitendo hicho.
Kwa upande wake muhudumu wa wodi namba saba ya wanawake na upasuaji Weru Kiula amesema walimpokea April 14 mwaka huu akiwa na hali mbaya ana vidonda kwenye makalio na mgongoni lakini kwa sasa anaendelea vizuri.
Afisa ustawi wa jamii hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga Prisila Mushi amesema matukio ya wanawake kupigwa na sungusungu yamekuwa yakitokea mara kwa mara na ameiomba serikali kuchukuwa hatua kali kwa watu waliohusika na ukatili huo.
Kamanda wa jeshi la polisi Mkoa wa Shinyanga Janeth Magomi amekiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kwamba wanawatafuta watu wote waliohusika na kumpiga viboko mwanamke huyo ambao walikimbia baada ya kufanya tukio hilo.
" Kweli tukio hili lipo na waliofanya tukio hili la kumpiga viboko mwanamke huyu tunaendelea kuwatafuta, ambao iimesemekana wamekimbia baada ya kufanya tukio hilo,"amesema Kamanda Magomi.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464