NSEKELA AONGOZA HARAMBEE SHULE ZA MARIAN, BAGAMOYO

   

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (kulia) akilisalimiana na Askofu Mkuu mstaafu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Kadinali Polycarp Pengo wakati alipowasili kwenye viwanja vya michezo vya Bongololo vya Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Marian mjini Bagamoyo, alipokuwa mgeni rasmi katika harambee ya kuchangisha fedha za ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Marian inayojengwa pamoja na zahanati, katika eneo la Mlingotini, wilayani Bagamoyo mkoa wa Pwani. Kushoto ni Mwanzilishi wa Shule za Marian, Father Valentino Bayo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela ameongoza harambee ya kuchangisha fedha za ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Marian inayojengwa pamoja na zahanati, katika eneo la Mlingotini, wilayani Bagamoyo mkoa wa Pwani.

Harambee hiyo iliyofanyika leo katika viwanja vya michezo vya Bongololo vya Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Marian mjini Bagamoyo ilisindikizwa na shughuli tofauti ikiwamo riadha, ibada maalumu ya kumshukuru Mungu pamoja na maonyesho ya wanafunzi.
Katika mchango wake, Nsekela alisema kuwa Benki ya CRDB imetoa Sh20 milioni kama sehemu ya mchango wa kufanikisha ujenzi huo huku yeye mwenyewe akichangia Sh10 milioni na marafiki zake wakitoa zaidi ya Sh10 milioni zitakazotumika kumalizia ujenzi wa madarasa shuleni hapo na miundombinu ya zahanati.


“Elimu ni moja ya kipaumbele cha Benki ya CRDB. Kila mwaka, tunatenga asilimia moja ya faida yetu baada ya kodi kusaidia utekelezaji wa miradi ya kijamii ikiwamo ya elimu na afya. Mwaka jana, tulitumia zaidi ya Sh366 milioni kwenye elimu na zaidiya Sh403 milioni kwenye afya. Tunafanya hivi tukiamini Serikali pekee haiwezi kukidhi mahitaji makubwa yaliyopo nchini hivyo ushiriki wa taasisi za dini na sekta binafsi ni muhimu,” amesema Nsekela.


Nsekela aliyekuwa mgeni rasmi kwenye harambee hiyo, alitoa mchango huo baada ya Father Valentino Bayo, mwanzilishi wa shule za Marian kumweleza kuwa jitihada zao za kuielimisha jamii hasa watoto wa mwambao wa Pwani zinakwama kidogo kutokana na ukosefu wa fedha.

“Sekondari ya Wasichana Marian ilijengwa Februari 1997 ili kuwapa fursa wasichana wa Mkoa wa Pwani na maeneo jirani kupata elimu bora. Mpaka sasa tumetanua huduma na sasa tunajenga Sekondari ya Wavulana hapa Mlingotini. Pia, tunajenga zahanati kuwahudumia wananchi. Ili kukamilisha miundombinu muhimu kwa huduma hizi, tuna upungufu wa fedha ambazo tunawaomba wadau mtusaidie kwa michango ya hali na mali,” alisema Father Bayo.


Baada ya harambee hiyo iliyokamilika kwa mafanikio, Mwalimu Super Vedasto, mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Marian Mlingotini aliishukuru Benki ya CRDB na wazazi waliojitokeza.


“Tunamshukuru Nsekela na marafiki zake kwa kujitoa kwao kufanikisha harambee hii. Wazazi na wananchi waliokuja leo wametupa faraja na tunaamini tutafanikiwa kukamilisha ujenzi huu hivyokutoa elimu bora kwa vijana wetu,” amesema Mwalimu Vedasto.

Naye Askofu Mkuu mstaafu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Kadinali Polycarp Pengo aliyeshiriki harambee hiyo aliipongeza Benki ya CRDB kwa kujitoa kushirikiana na kanisa kuboresha huduma za jamii.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (kulia) akizungumza jambo na Askofu Mkuu mstaafu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Kadinali Polycarp Pengo, wakati wa harambee ya kuchangisha fedha za ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Marian inayojengwa pamoja na zahanati, katika eneo la Mlingotini, wilayani Bagamoyo mkoa wa Pwani leo.

Sehemu ya wanafunzi waanzilishi wa Shule za Marian, wakiwa katika hafla hiyo.
Sehemu ya wanafunzi wa sasa wa Shule za Marian.
Burudani kutoka kwa Wanafunzi.



Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela akimkaidhi hundi kwa Mwanzilishi wa Shule za Marian, Father Valentino Bayo.




Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464