WAKAZI WA MBARALI WAIPONGEZA SERIKALI KWA MATIBABU YA MACHO
Na. WAF, Mbarali
Wakazi wa Mbarali wameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Afya na wadau wa huduma za macho kwa kuwapatia matibabu ya macho bila malipo.
Akizungumza katika kambi ya upasuaji wa mtoto wa jicho inayoendelea kwenye hospitali ya Wilaya Mbarali Bw. Antony Ndwenywa(83) kutoka kitongoji cha Mkanyageni-Rujewa ambaye alifanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho macho yake mawili mwezi Disemba 2022, amesema tangu amefanyiwa upasuaji anaendelea vizuri na hivi sasa anasoma hata magazeti.
"Mimi nilifanyiwa macho yote mawili yalikuwa na mtoto wa jicho na hadi sasa naendelea vizuri.Tunaishukuru Serikali kwa kutupatia huduma sisi watu wa chini ,huduma hizi ni bila malipo ninashukuru sana.
Naye, Bi. Vailet Mbelewele mkazi wa Mabadaga ambaye alikua na mtoto wa jicho kwa muda wa mwaka mmoja amewashukuru watoa huduma wakiwemo madaktari na wauguzi kwa huduma nzuri walizompatia na kuongeza kuwa ametolewa bandeji na sasa anaona.
Amesema mara baada ya kupata tatizo hilo alikua akinunua dawa kwenye maduka bila ushauri wa madaktari "nawashauri wananchi wasijinunulie dawa mje moja kwa moja kwani madaktari wapo na huduma ni nzuri".
Vilevile Mzee Ahmed Abdallah Mkazi wa Igurusi ambaye alishakwisha fanyiwa upasuaji wa jicho moja miaka miwili iliyopita na kwa kambi hii amefanyiwa upasuaji jicho la pili amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan pamoja na viongozi wake wa chini kwa jitihada zake kwa kuwasaidia watu wa chini.
"Tunamshukuru Mama kwa kutusaidia mambo mengi kama barabara,ametuletea mbolea,natoa sifa kwa Dkt. Samia anatuhudumia sisi watu wa hali hii kwani habagui na hachagui.
Kambi ya upasuaji wa mtoto wa jicho wilayani Mbarali imeanza tarehe 11 Aprili,2023 na inatarajiwa kumalizika tarehe 20 Aprili,2023.Inaratibiwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la Hellen Keler International la hapa nchini.