WAKRISTO WAMETAKIWA KUSIMAMA IMARA NA KUISHI MAISHA MATAKATIFU


Mchungaji Edward Mtinda ambaye pia ni mwinjilisti akiombea kanisa na Taifa kwa ujumla


Suzy Luhende Shinyanga Blog

Mchungaji na mwinjilisti wa kanisa la Tanzania Assemblies of God TAG Mwanza Edward Mtinda amewataka wakristo wote kuishi maisha matakatifu, kuwa imara mbele za Mungu na kuacha kuyumbishwa yumbishwa na shetani mara kwenda kwa waganga mara kanisani.

Hayo ameyasema kwenye ibada ya Pasaka  wakati akihubiri neno la Mungu katika kanisa la Philadelfia lililoko kata ya Ndembezi manispaa ya Shinyanga, ambapo amewataka waumini wa kanisa hilo kusimama imara, kujitoa kufa na kupona kuyafanya mapenzi ya Mungu.

Mchungaji Mtinda ambaye pia ni mwinjilisti wa kimataifa alitoa ujumbe unaosema Kanisa lililojengwa juu ya Mwamba,na kusoma neno kutoka mathayo 7:24-29 ambapo amewataka waumini wote waliomwamini kristo wasimame imara wasitikisike kwa sababu ramani ya kanisa ni Yesu mwenyewe, mjenzi wa kanisa ni Yesu mwenyewe mmiliki wa kanisa ni Yesu na mchungaji wa kanisa ni Yesu mwenyewe.

"Kanisa lililojengwa juu ya mwamba ni kanisa tendaji, kanisa lenye kujitoa kufa na kupona kuyafanya mapenzi ya Mungu na lenye msimamo halitikisiki wala kuyumbishwa ambalo linadumu katika neno na kukataa mafundisho ya uongo na kushinda majaribu maovu,"amesema Mchungaji Mtinda.

Aidha amesema ili mkristo aweze kuishi maisha matakatifu na kuwa imara mbele za Bwana yahitajika macho ya kiroho ambayo yanaona vitu vitatu yanaona hatari ya dhambi, yanaona faida ya kuishi maisha ya usafi wa kiroho na yanaona hasara ya kukosa ibada.

"Yesu akasema hadharani akamwambia Petro kwamba nyumba itajengwa na mimi mwenyewe na kanisa linatenda kazi ya Mungu na kanisa hilo ni moto unaowaka ndani hadi malengo ya Mungu yatimie, ambalo limevikwa uwezo, mamlaka na nguvu za Mungu,"amesema Mtinda.

Pia amesema matokeo ya uponyaji wa watu na Taifa unapatikana, roho ya udunia na ufalme wa giza kuvunjwa, "neno la Mungu linasema kila asikiaye neno langu na kulifanya anafananishwa na mtu aliyejenga nyumba juu ya mwamba,"amesema.

Mtinda amesoma neno hilo Mathayo 7:24-29 inasema basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba, mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba.

Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga, mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa, Ikawa, Yesu alipoyamaliza maneno hayo, makutano walishangaa mno kwa mafundisho yake, kwa maana alikuwa akiwafundisha kama mtu mwenye amri, wala si kama waandishi wao.

Kwa upande wake mchungaji Kiongozi wa kanisa la Philadelfia lililoko kata ya Ndembezi manispaa ya Shinyanga Baraka Laizer amewaomba waumini wote wa kanisa hilo kusimama imara wasikubali kuyumbishwa yumbishwa wakatae mafundisho ya uongo, ili waweze kuuona ufalme wa mbinguni.
Mchungaji Edward Mtinda akihubiri katika kanisa la Philadelfia 
Mchungaji Baraka Laizer akiomba
Mchungaji Edward Mtinda akiendelea kuhubiri neno la Mungu
Waumini wa kanisa la Philadelfia wakimsifu Mungu
Waumini wa kanisa la Philadelfia wakisikiliza neno la Mungu
Waumini wa kanisa la Philadelfia wakiomba
Kwaya ya kanisa la Philadelfia ikimsifu Mungu 
Kwaya ya kanisa la Philadelfia ikimsifu Mungu 
Kwaya ya kanisa la Philadelfia ikimsifu Mungu 

Kwaya ya kanisa la Philadelfia ikimsifu Mungu 
Kwaya ya kanisa la Philadelfia ikimsifu Mungu 
Kwaya ya kanisa la Philadelfia ikimsifu Mungu 
Kwaya ya kanisa la Philadelfia ikimsifu Mungu 
Mtenda kazi wa kanisa la Philadelfia Advert akimsifu Mungu 






Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464